Astronomia Kwa Kiswahili

 

Rudi - Home 

Unakaribishwa kufaidi Anga za Tanzania

Na Dkt. Noorali T. Jiwaji

Namna Ya Kuelewa Nyota Za Mbinguni

Astronomia ni utaalamu wa nyota, sayari na nyendo zake. Watu wengi huvutiwa na maelezo na mazungumzo yanayohusu mambo ya nyota. Wakibahatika kuona tukio fulani la ajabu mbinguni pia wanavutiwa sana. Lakini papo hapo, wengi wao hushindwa kuelewa mambo hayo kwa undani.

Ni muhimu kujifunza kuhusu nyota kwa sababu tunaweza kuelewa umbo na mwenendo wa Dunia yetu na kuelewa namna tabia ya hali ya hewa Dunia yetu ilivyobadilika katika mamilioni ya miaka iliyopita. Tunaweza kujifuza kuhusu chimbuko la mfumo wa Juan na sayari zake na hata wa ulimwengu (universe) wenyewe, na kufikiria kuhusu namna nyingine za maisha zinazoweza kuwepo ulimwenguni.

Tunaweza kujifunza kuhusu vitu vingi vya ajabu vilivyopo ulimwenguni, kama vile nyota za mbali sana zinazotoa mawimbi ya redio yenye nguvu kali mno na nyota za nutroni. Pia kuna sehemu za anga ambazo zinauwezo wakuvuta hata mwanga ndani yake (BLACK HOLES). Pengine kwa kuelewa elimu ya Astronomia tutaweza kuthamini na kuelewa ukubwa wa ulimwengu wetu kuipana na kiumri.

Duniani tunaweza kuelewa mvuto wa Jua na Mwezi juu ya Dunia yetu ambao huleta kujaa na kupwa kwa maji baharini. Tutaweza kuelewa kwamba kupatwa kwa Jua na Mwezi si mazingaombwe ya waganga au wanajimu lakini ni matukio yaliyo na sababu maalum inayoeleweka - yaani hutokea kwa sababu Mwezi na Dunia zinaizunguka Jua.

Je Tutaanzaje?

Nyota ni ngumu kuzielewa kwa sababu ziko mbali mno na sisi na hatuwezi kuzifikia kwa njia yoyote. Mojawapo ya njia rahisi ya kukielewa kitu ni kwa kukiangalia kwa makini. Kwa bahati mbaya ukianza kuangalia nyota za angani, utakuta zinaleta picha ya min'garo na mimeremeto zilizokaa shaghalabaghala bila mpangilio wowote. Ukiongezea matatizo utakayopata kutokana mawingu kufunika nyota mara kwa mara, hutalaumiwa ukikata tamaa kabla hata hujaanza! Lakini amini usiamini, kuna utaratibu maalum wa kimsingi unaoweza kuutumia kuelewa mpangilio wa nyota. Na kama utakuwa makini na mvumilivu, utaweza kujifunza namna ya kutambua nyota nyingi pamoja na kutofautisha maumbo mbali mbali yanayoonekana angani. Ukielewa namna ya kutambua nyota, basi utakuwa umejipanulia uwezo wako wa kuelewa elimu nzima ya Astronomia na hatimaye ya ulimwengu wetu.

Je, ni lazima kutumia darubini za hali ya juu kutazamia mbinguni? Hapana. Macho yetu yanatosha kuanza kuelewa na kufurahia mbingu zetu za usiku. Iwapo kuna darubini, zinaweza kutumiwa kuchunguzia milima na mabonde yaliyopo mwezini. Iwapo utapenda kuona mambo mengi na kwa undani zaidi kwenye sayari, utahitaji darubini kali (telescope).

Kutambua nyota na Makundi ya Nyota

Angani, nyota zote zimejipanga kwa mfumo ambao haubadiliki. Lakini kuna vitu vingine kwa mfano Mwezi, sayari mbali mbali, vimondo (comets) na vinginevyo vinavyobadilisha nafasi zake angani siku hadi siku. Ni muhimu sana kwanza kutambua na kuuelewa mandhari ya mfumo wa nyota ambayo haibadiliki. Lakini kwa kutazama tu mara moja moja angani utashindwa kutambua mfumo wowote.

Kuna tatizo gani? Kwanza, mawingu yanaelekea kuziba nyota nyingi mara kwa mara. Hata hivyo sababu ya msingi ni kwamba mfumo wa mpangilio wa nyota husogea magharibi kila saa kutokana na mzunguko wa Dunia kwenye mhimili wake (zingatia kuwa mzunguko huu ni kama ule unaosababisha Jua kusogea angani asubuhi hadi jioni). Sababu ya tatu ya kubadilika kwa mandhari ya nyota ni kwamba nyota zote husogea mgharibi pole pole siku hadi siku, kufuatana na mzunguko wa Dunia kuizunguka Jua mara moja kwa mwaka.

Kwa hiyo ukitaka kutambua maumbo ya nyota katika mandhari ya anga za usiku, hakikisha unaangalia vizuri sehemu moja ya anga saa ile ile kwa siku chache mfululizo. Huna budi kuchagua sehemu nzuri ambapo sehemu hiyo ya anga haizuiliwi mno na miti au vizuizi vingine. Si wote tuliyo na muda wa kuangalia anga kwa makini kila siku. Na pamoja hiyo, hali ya hewa inaweza kutuzuia kuangalia nyota vizuri. Kwa hiyo hatuna budi kuzingatia mwendo ule wa pole wa kusogea magharibi kwa umbo la mbingu baada ya siku kadhaa. Inabidi kuiangalia sehemu hiyo hiyo ya anga saa moja kabla kila baada ya majuma mawili.

Kama utafauta kanuni hizi za msingi (ingawa zinatumia muda sana!), utaweza kutambua maumbo machache ya muhimu. Upande mzuri wa kuangalia mbingu hapa kwetu Tanzania ni upande wa kusini ambako kuna nyota nyingi na maumbo mengi yanayoweza kutambulika kwa urahisi.

Jambo la msingi ni kutambua maumbo sanifu yanayojulikana kuwa ni Makundi Ya Nyota (constellations). Kwenye anga la mbingu ya kusini utaweza kupata umbo kama tiara au kishada la nyota nne zijulikanazo kama ni “Msalaba wa Kusini”. Iwapo utaangalia kwa muda wa saa chache usiku huo huo, utatambua kwamba upande mrefu wa msalaba daima unaelekea kusini. Umbo jingine la kuvutia unaloweza kulitambua upande wa mashariki kwa sehemu ya tosini. Hili ni kundi la nyota lijulikanalo kuwa ni NG’E, kundi la nyota lenye umbo la ng’e ambalo limeundwa na nyota tatu au nne zinazo unda “kichwa” chake na nyota yenye mwanga mkali mwekundu ijulikanayo kama ANATARES kwenye “shingo” yake. Na mfuatano wa nyota nyingi huunda “mkia” wake na kumalizia na nyota mbili zilizokaribiana zinazounda “mwiba”. Linganisha unachokiona mbinguni na ramani rahisi ya nyota iliyoonyeshwa hapa. Ili uweze kuitumia ramani hii iishike wima na kuizungusha ili upande unaoelekea unasomeka chini. Mara baada ya kutambua umbo au kundi moja, ramani kama hizi zinaweza kukuongoza kutafuta maumbo mengine angani na hatimaye kutambua nyota zote angani. Jaribu kutambua angalau umbo moja la nyota kila wakati unapoweza kuona mbingu kwa urahisi, na hatimaye utaelekea kupenda elimu ya nyota kwa ukamilifu.

Maelezo Machache Ya Jinsi Ya Kutumia Ramani Ya Nyota

Iwapo ramani iliyochapwa ni ndogo, ikuze nakala kivuli asilimia 200, na tumia nakala hiyo kwa kuainisha nyota na Makundi ya nyota. Tafuta eneo unaloweza kuona vizuri sehemu kubwa ya mbingu kuanzia kwenye upeo wa macho hadi utosini. Tafuta mwelekeo wako wa wastani kwa kutumia Jua wakati wa mchana na zoea eneo lako. Ifikapo kiasi cha saa 2 usiku, uelekee upande uliochagua na iishike wima ramani ya mbingu na igeuze hadi upande unaoelekea unasomeka chini katika ramani.

Yazoeze macho yako kwa dakika tano au kumi na kinga macho yako kutokana na mwanga wowote mkali unaoweza kuwa upande unaoangalia. Tumia tochi yenye mwanga hafifu kumulika ramani. Nyota zilizoko karibu na ukingo wa mzingo katika ramani zitaonekana angani karibu na upeo wa macho wa upande unaoelekea. Nyota zilizopo katikati katika ramani ni zile

zitakazoonekana utosini. Zingatia kwamba katika ramani zimeonyeshwa nyota zile zile tu zenye mwanga mkali, lakini uhakika wa kuonekana nyota angani utategemea hali ya mwanga katika eneo lako. Watazamaji walioko katika miji mikubwa kama Dar es Salaam wataona nyota chache zaidi kwa vile mwanga mkali wa mji utang’arisha anga na kufunika mwanga wa nyota hafifu. Lakini watu wanoishi mbali na mji wanaweza wakaona nyota nyingi zaidi kuliko zile zilizoonyeshwa katika ramani kwa vile anga huwa nyeusi kabisa sehemu hizo.

Kumbuka kwamba ukibadilisha mwelekeo, zungusha ramani pia huku ukiwa umeishika wima na hakikisha kwamba upande unaoelekea upo chini katika ramani.

Nakutakia utazamaji mwema wa nyota.

Rudi - Home