Matukio Mahususi ya Astronomia Tanzania kwa Mwaka 2017

Matukio Mahususi ya Astronomia Tanzania kwa Mwaka 2017


 

 

·         Kupatwa kwa Jua na Mwezi –    Jumla ya mara nne kutapatwa.  Mara tatu kati  ya hizo

                                zitaonekana hapa Tanzania kama ifuatayo:

1.       Kupatwa kwa Mwezi wenye kivuli chepesi usiku wa manane tarehe 10 Februari kwenda Februrari 11, kuanzia saa 7:34 – 11:53 alfajiri.

2.       Kupatwa kwa Jua Sehemu, tarehe 26 Februari kuanzia saa 12:32 jioni hadi saa 1:08 usiku.

3.       Kupatwa kwa Mwezi Sehemu, tarehe 7 Agosti kuanzia saa 2:33 hadi saa 4:18 usiku.

·         Sayari – Sayari tano zitaonekana kwa uwazi, ambazo ni Zebaki(Mercury), Zuhura(Venus), Mirihi(Mars), Mushtarii(Jupiter), na Zohali(Saturn)

 

·         Jua na Mwezi:

1.       Awamu za Mwezi, Mwezi Mwandamo na Mwezi Mpevu

2.       Siku Mlingano(Equinox) na Solistasi – Jua linapokuwa utosini Ikweta na kuwa kaskazini na kusini kabisa mwa Ikweta.

·         Nyota, Vimondo, Vimondo mkia

1.       Nyota angavu zaidi za mwaka mzima.

2.       Mwezi kufunika nyota tarehe 12 Februari, 13 Machi na 31 Mei.

3.       Vimondo vya mfululizo – Matukio makubwa kwa anga letu ni siku chache kabla na baada ya tarehe 6 Mei (Eta Aquarids) na Desemba 14 (Geminids).

4.       Vimondo mkia – Vimondo mkia vitatu vinaweza kuwa angavu na kuonekana tarehe 11 Februari, 15 Mei na 15 Juni katika sehemu zenye giza nene hasa kwa kuangaliwa kwa darubini

·         Setelaiti

Chombo cha Anga cha Kimataifa (ISS) na satelaiti nyingi zinaonekana mara nyingi mwaka mzima.

 


Picha ya mabadiliko ya pete za Zohali imetolewa kutoka tovuti ya:
https://astrobob.areavoices.com/2015/06/28/egg-moon-close-to-saturn-tonight-occults-theta-librae/

 

Kutakuwa na KUPATWA mwaka huu, na tatu kati ya hizo zitaonekana Tanzania.  Kupatwa kwa kwanza kutakuwa wa Mwezi wenye kivuli chepesi, usiku wa manane Februari 10 kuelekea Februari 11, kuanzia saa 7:34 hadi saa 11:53 alfajiri.  Kutatupa changamoto ya kutambua uweusi wa kivuli chepesi cha Dunia kitakachofunika Mwezi.  Tarehe 26 Februari kuanzia saa 12:32 jioni hadi kuchwa kwa Jua saa 1:08, watazamaji wa kanda za kusini wataona Jua likipatwa kwa sehemu ndogo ya Jua.  Ingawa hakutakuwa na msisimko kama ule wa mwaka jana wa kupatwa kwa Jua Kipete, bado ni tukio la kupendeza kufuatiwa na waakazi wa kanda za kusini.  Kupatwa kwa tatu utakuwa kupatwa kwa Mwezi Sehemu tarehe 7 Agosti kuanzia saa 2:3 usiku hadi saa 4:18 usiku ambapo sehemu ndogo ya Mwezi utafunikwa na kivuli cha Dunia. Kupatwa kwa mwisho mwaka huu ni kupatkwa Jua Kamilifu tarehe 21 Agosti ambako hakutaonekana hapa Tanzania, ila kutatokea Marekani kote.  Iwapo utabahatika kutembelea huko wakati wa kupatwa usikose kuangalia tukio hili la kusisimua.

 

Kwa upande wa SAYARI, mwaka ulianza na mstari wa vitu angavu – Mwezi hilali, Zuhura na Mirihi. Vinavyoonekana dhahiri kwa muda wa siku kadhaa karibu na upeo wa magharibi.  Mwezi, Zuhuru na Mirihi zimekusanyika pamoja tena 31 Januari, na mpangilio huo unaendelea mpaka tarehe 3 Februari.  Halafu tena, mwisho wa mwezi wa Februari, tarehe 28, sayari hizi zinakusanyika pamoja ingawa si kwa ukaribu, karibu na upeo wa magharibi, mara baada ya machweo.

 

Jozi ya Zuhura na Mars inaendelea kuonekana kwa pamoja kwenye anga jioni upeo wa magharibi mwezi wote wa Februari, huku jozi ikisogea upande wa kulia siku hadi siku.

 

ZOHALI (Venus) - Kusema kweli Zuhura ni sayari ang’avu ya kupendeza wakati huu, iking’ara kama nyota ya jioni na kufikia mwinuko wa juu zaidi wa nyuzi 45 angani, juu ya upeo wa magharibi, sasa inaingia awamu ya Mwezi Mwandamo na kuonekana kwenye darubini kama hilali pana.  Hilali hii ya Zuhura itazidi kuwa nyembamba na wa ukubwa wa zaidi ya mara mbili kadiri sayari hiyo inavyokaribia Dunia.

 

Baada ya hapo, Zuhura itaingia ukingoni kama nyota ya alfajiri na kufikia mwinuko wake wa juu kabisa juu ya upeo wa mashariki Mei katikati.  Itaendelea kuonekana kabla ya mpambazuko mpaka katikati ya Desemba.  Mwezi Novemba tarehe 17, Zuhura itaunda utatu wa pamoja na Mwezi Mwandamo (hilali), Mustarii ang’avu, na Zuhura inayong’ara.  Utatu huu wa Mwezi, Mushtarii na Zuhura utatoa mwonekano wa kustaajabisha.   Mwisho wa mwaka Zuhura itapotea katika mng’aro wa Jua la machweo na Februari mwakani itaanza tena kuonekana kama nyota ya jioni katika mbingu za magharibi.  Kwa hiyo kwa kipindi cha mwaka mzima huu, Zuhura itakuwa katika mionekano mingi tofauti ya kuvutia pamoja na Mwezi Mwandamo katika anga ya magharibi wakati wa machweo na mwishoni katika mbingu ya mashariki wakati wa mawio.   Tembelea www.AstronomyinTanzania.or.tz kwa tukio moja moja la Zuhura na sayari zingine na nyota kwa mwaka mzima.

 

MIRIHI (Mars) - Hivi sasa Mirihi inaonekana kama nyota nyekundu inayong’ara kama sayari ukiilinganisha na nyota ambyo humeremeta.  Mirihi inaonekana mara baada ya machweo karibu sana na Zuhura inayong’ara nusu juu ya anga ya magharibi.  Itaendelea kuonekana mpaka katikati ya Juni ambapo itakuwa karibu zaidi na Jua linalokuchwa.  Kuanzia mwisho wa Agosti Mihiri itaonekana kwenye anga ya asubuhi juu ya upeo wa mashariki, ikiinuka polepole angani siku hadi siku.  Ifikapo mwanzoni mwa Desemba Mirihi itajipanga mstari na Zuhura, Mushtarii, Mwezi Mwandamo hilali na nyota ya Spica kuanzia mwanzoni mwa Desemba hadi katikati ya Desemba.  Kwa hiyo Mirihi pia itatoa vivutio vingiangani mwaka huu.

 

ZEBAKI (Mercury)  ni sayari yenye utata na kujificha na si rahisi kuona bila kuazimia kwa vile daima inakuwa karibu sana na Jua, kwa hiyo ni lazima uitafute wakati iko juu sana angani.  Hii itatokea mara mbili kwenye anga la magharibi wakati wa machweo, tarehe 1 Aprili na tarehe 30 Julai, na mara mbili kwenye anga la mashariki wakati wa mawio, tarehe 17 Mei na tarehe 22 Septemba.  Mwinuko wa juu kabisa ni nyuzi 27.  Mnamo tarehe 17 Mei na 30 Julai ni muda muafaka wa kuangalia Zebaki.  Nyakati zingine inapokuwa karibu na Mwezi hilali, au Zuhura inaweza pia kuonekana kwa urahisi.  Matukio hayo unaweza kupata kwa kutembelea tovuti ya “Astronomy in Tanzania”.

 

MUSTARII (Jupiter) ni sayari kubwa sana na angavu zaidi na unaweza kudhani ni Zuhura ukiiona angani.  Namna ya kuzitofautisha yota hizi mbili angani ni kwa kuona kuwa Zuhura ama iko karibu na upeo wa magharibi mara Jua linapozama au karibu na upeo wa mashariki kabla tu ya Jua kuchomoza.  Zuhura haiwezi kamwe kuonekana utosini mwa anga. Mustarii inaweza kuonekana upande wowote angani kati ya mashariki na magharibi, kwa hiyo Mustarii inaweza kuonekana utosini na hii hutumika kutofautisha kati ya Zuhura na Mushtarii.

 

Kwa sasa Mushtarii iko utosini kwenye anga la asubuhi na itaanza kuonekana jioni kuanzia mwisho wa Februari ikijichomoza usiku wa saa nne hivi katika anga ya mashariki.  Ifikapo tarehe 7 Aprili, Mushtarii itajichomoza kwenye upeo wa mashariki wakati wa machweo, huku Jua likizama upande wa magharibi.  Hii inamaanisha kwamba uso wa Jupita unaangazwa moja kwa moja na mwanga wa Jua.  Hali hii huitwa “kukabiliana” (conjunction) na sayari ya Mushtarii inang’aa sana wakati huu ambayo utaona siku ya tarehe 7 Aprili.

 

Siku zitakavyo pita, Mushtarii itaonekana juu zaidi katika anga la  mashariki kila baada ya machweo.  Itaendelea kupanda juu siku hadi siku hadi kufikia utosini na baada ya hapo kwenda upande wa anga la magharibi.  Kufikia mwezi Oktoba, Mushtarii itakuwa jirani na upeo wa magharibi na kufikia tarehe 26 Oktoba, itakuwa upeoni karibu kabisa na Jua linalozama ambayo huitwa “mwingiliano”.  Baada ya hapo kuanzia katikati ya Novemba Mustarii itaonekana kwenye anga la asubuhi karibu na upeo wa mashariki wakati wa machweo.  Mushtarii itanonesha matukio mengi ya kukumbukwa mwaka mzima huu, hasa itakuwa karibu na sayari zingine na Mwezi na nyota angavu.  Angalia www.AstronomyinTanzania.or.tz kwa maelezo zaidi kuhusu tarehe, nyakati na mahali pakuangalia matukio haya.

 

Kwa kutumia darubini ya kawaida tu, Mustarii inaonesha mikanda sambamba ya mawingu na miezi minne inayobadilisha nafasi kila siku na hata kila saa.  Wakati mwingine miezi hiyo hufichwa nyuma na tufe la sayari na nyakati nyingine vivuli vya miezi vinaweza kuonekana kwenya uso wa sayari kwa kutumia darubini nzuri.

 

ZOHALI (Saturn) ni sayari yenye pete.  Nayo huonekana kwa uwazi mzuri angani, iking’ara kwa mwanga si mkali sana, ni sayari inayopendeza mno kuangalia kupitia darubini, na kuonesa mfumo wa pete bapa.  Mwaka huu pete hiyo inaonekana vizuri zaidi kwa sababu pete imeinama kuelekea kwetu na kujionesha kiasi cha kuridhisha sana.  Zohali kwa sasa inaonekana wakati wa asubuhi nusu juu angani kutoka upeo wa mashariki kabla ya machweo.  Zohali itaanza kuonekana nyakati za usiku ikichomoza kuanzia saa nne hivi mwanzoni mwa Mei na kuendelea. Itafikia hali ya “kukabiliana” na Jua na kuonekana kwa ung’avu zaidi tarehe 15 Juni.  Siku hiyo Zohali itachomoza upande wa mashariki nyakati za machweo, Jua linapokuchwa upeo wa magharibi.  Katika kukabiliana uso kamili wa Zohali unamulikwa na Jua na kufanya ionekane vizuri zaidi.  Baada ya hapo Zohali itapanda pole pole juu ya anga la mashariki na kwenda utosini hadi kufikia upande wa magharibi katika siku na miezi inayofuata.  Ifikapo Septemba itakuwa kwenye anga la magharibi na kumaliza mwaka ikiwa karibu zaidi na upeo wa magharibi jirani na Jua.  Mwanzoni mwa Desemba itapotea nyuma ya mng’aro mkali wa Jua.  Kwa hiyo Zohali nayo itakuwa na matukio mengi ya kukumbuka mwaka mzima wakati itakapoonekana karibu na Mwezi na sayari mbali mbali.  Maelezo kamili ya matukio hayo ya Zohali unaweza kupata kwenye tovuti ya www.AstronomyinTanzania.or.tz..

 

JUA ni nyota iliyojirani zaidi kuliko zingine, nalo litaonesha mwendo wake dhahiri mwaka mzima, likienda nyuzi 23.5 kaskazini na kusini mwa Ikweta.  Litakuwa juu ya anga za maeneo ya Ikweta tarehe 20 Machi na 22 Septemba.  Tarehe hizo hujulikana kuwa ni “siku mlingano” na muda wa usiku na wa mchana hulingana kutokana na kwamba Ikweta iko moja kwa moja kwenye ubapa wa Mfumo wa Jua, kwa hiyo Jua linaangaza kwa ulinganifu kwenye Dunia.  

 

Kutokana na mwinamo wa mhimili wa mzunguko wa Dunia kwenye ubapa wa Mfumo wa Jua kwa nyuzi 23.5, Jua huangaza wima kwenye latitude 23.5 kaskazini (Tropic of Cancer) Juni 21.  Hii inafahamika kuwa ni “solistasi ya kaskazini”, wakati inapokuwa joto kaskazini na baridi kusini mwa Dunia.  Halikadhalika Jua linawaka wima kwenye latitude 23.5 kusini (Tropic of Capricorn) Desemba 21, na kuitwa “solistasi ya kusini”, na kusababisha msimu wa joto kusini na msimu wa baridi kaskazini.  Kuanzia Machi 20 hadi Septemba 22, mchana ni masaa mengi kuliko usiku sehemu za kaskazini wakati upande wa kusini usiku ni masaa mengi kuliko mchana.  Kinyume chake hutokea kuanzia Septemba 22 hadi Machi 20.  Hapa Tanzania maeneo tunayoishi sisi hakuna tofauti kubwa kati ya muda wa mchana na wa usiku kwa vile tuko jirani sana na Ikweta, kwa hiyo usiku na mchana ni karibu muda sawa mwaka mzima na hali ya joto pia inkuwa sawa mwaka mzima.

 

MWEZIi nao unabadili umbo lake kwa awamu, kuanzia Mwezi Mwandamo (hilali), Nusu Mwezi, na Mwezi Mpevu kwenda tena Nusu Mwezi na kurudia Mwezi Mwandamo kila mzunguko wa Mwezi kuizunguka Dunia. Miezi mwandamo mwaka huu itakuwa 28 Januari, 26 Februari, 28 Machi, 26 Aprili, 25 Mei, 24 Juni, 23 Julai, 21 Agosti, 20 Septemba, 19 Oktoba, 18 Novemba, na 18 Desemba. Miezi mpevu itakuwa Januari 12, Februari 11, Machi 12, Aprii 11, Mei 11, Juni 09, Agosti 07, Septemba 06, Oktoba 05, Novemba 04, na Decemba 03.  Robo ya kwanza, na robo ya mwisho wakati ambapo Mwezi huwa na umbo la nusu Mwezi itatokea kati ya Mwezi Mwandamo na Mwezi Mpevu katika kila mzunguko. Angalia muda kamili hapa.

 

Siku za mapumziko zinazotegemea mizunguko ya Mwezi nazo zitaamuliwa kwa msingi wa tarehe za Mwezi Mwandamo kwa vile mwezi wa Kiislamu unaanzwa baada ya kuona hilali ya kwanza ambayo hotokeza siku moja au mbili baada ya kuandama kwa Mwezi kutegemeana na mwinuko wa Mwezi juu ya Jua linalotua chini ya upeo wa magharibi.  Kwa hiyo tarehe za Idd-ul-Fitri zinaweza kutarajiwa 25 Juni au 26 Juni, na Idd-ul-Hajj inatarajiwa tarehe 1 au 2 Septemba.  Sikukuu ya Maulidi itakuwa Desemba 1 au 2.

 

Miongoni mwa VIMONDO MFULULIZO (Meteor Showers) tisa (9) vya kawaida Duniani kila mwaka, vitakavyoonekana vizuri na kufaa kuangalia hapa kwetu katika maeneo karibu na Ikweta na kwa kusini ni viwili.  Siku chache kabla na baada ya tarehe 6 Mei vitaonekana vimondo vya “Eta Aquarids” na tarehe 14 Desemba ni vimondo vya “Geminids”.  Muda mzuri zaidi kuangalia vimondo hivi baada ya saa sita usiku wa manane hadi kabla ya alfajiri.  Wakati huo, mzunguko wa Dunia kulizunguka Jua huelekea na kugonga chembe chemba za vumbi zilizoachwa nyuma na vimondo vya mkia vilivopita hapo zamani.  Chembe chembe hizo zinapogonga hewa ya anga la Dunia huungua na mwanga wake huonekana usiku.  Mwezi nao lazima uwe chini ya upeo ili kuwa na giza ya kutosha kuweza kuangalia vimondo vingi zaidi.   Njia nzuri ya kuona vimondo hivi ni kulala chali chini katika mkeka na kuangalia juu anga lote bila taabu.  Kwa maelezo zaidi na muda na mahala pakutokeza vimondo, angalia tovuti ya “Astronomy in Tanzania”.

 

VIMONDO MKIA (Comets) vinakuwa amilifu zaidi wakati vinapokuja karibu na Jua katika mizingo yake mduaradufu kama umbo la yai, joto la Jua linavukiza maji yaliyoganda na kubakisha tone la vumbi angavu. Kiasi fulani cha vumbi husukumwa nje ya tone na msukumo wa mwanga wa Jua, na inaunda mkia wa kimondo hicho.  Vimondo mkia vitatu vinaweza kuwa angavu mwaka huu na kuonekana kwenye anga za giza la kutosha tarehe 11 Februari (“comet 45P/Honda”),  15 Mei (“comet C/2015 ER 60 PanSTARRS”) na tarehe 15 Juni (“comet c/2015 V2 Johnson”).  Hasa zinapoangaliwa kwa kutumia darubini zitaonekana vizuri zaidi.  Kwa maelezo zaidi hasa karibu na tarehe husika peruza tovuti ya “Astronomy in Tanzania”.

 

MWEZI hufunika nyota mara moja moja unapopita mbele ya nyota fulani, na kuziba upeo wetu wa kuona hiyo nyota na kusababisha nyota ipotee angani kwa muda.  Matukio matatu ya Mwezi kufunika nyota yatatokea mwaka huu. Tarehe 12 Februari  nyota ZC1547 itafunikwa na Mwezi, tarehe 14 Machi nyota X54027 na nyot ZC1821 zitafunikwa na Mei 31 nyota ZC 1487 itafunikwa.  Kwenye tovuti ya www.AstronomyinTanzania.or.tz utapata nyakati kamili na mahali pakuangalia kufunikwa nyota hizo.

 

SETELAITI zinazozunguka Dunia huleta furaha sana kufuatilia na kuangalia angani kwa vile zinaonekana kama nyota zinazotembea.  Iwapo unaangalia kwa makini na kuchunguza anga la utosini baada ya giza kuingia mara baada ya machweo utaona kitone kama nukta ikisogea pole pole angani kati ya nyota zilizotulia.  Hizi ni setelaiti na zinaonekana kutokana na mzingo wa setelaiti ni juu sana na mwanga wa Jua unaweza kufikia kwenye setelaiti wakati Dunia inakuwa na giza. Mwanga huo wa Jua unaakisiwa na satelaiti na kufikia kwetu na tunaziona.  Baadhi ya satelatiti huangaza zaidi ya nyingine, wakati nyingine huangaza na kuzima.  Setelaiti yenye kung’aa sana ni Kituo cha Anga cha Kimataifa (International Space Station – ISS) kinachozunguka kwa umbali wa kilomita 400 juu ya uso wa Dunia.  Kinang’ara kwa kiwango mkali sana kama ndege, hata kuzidi Zuhura mara nyingine, ingawa husafiri polepole kwenye anga.  Setelaiti nyingine ni “Hubble Space Telescope” (HST) na inayowaka na kuzima ni “Iridium Flares”.  Muda na mahali pakuangalia setelaiti hizi angani hutegemea mahali ulipo.  Unaweza kutumia tovuti kwenye mtandao kubaini nyakati halisi na mielekeo ya setelaiti hizo.  Tembelea tovuti ya www.heavens-above.com kwa melezo zaidi kuhusu setelati zote na nyakati za kuangalia hizo na mielekeo yao.  Kwa setelaiti ya ISS ambayo ni setelaiti angavu zaidi na inafurahisha kufuatilia na kuwaonesha marafiki zako unaweza kuipata kwenye tovuti ya “Spot the Station” ya NASA unayoweza kupata kwenye Google na kufuata maelekezo kwenye tovuti hiyo na kuchagua kati ya Dar es Salaam au Mwanza au mji wa jirani na ulipo. 

 

Tembelea www.AstronomyinTanzania.or.tz kwa taarifa za mara kwa mara kuhusu wapi na lini uangalie setelaiti, nyota, sayari, na matukio mengine.  Furahia kuona matukio mengi ya kusisimua ya kiastronomia mwaka huu wa 2017.

 Note:

Orodha kubwa zaidi ya matukio ya astronomia Duniani inapatikana katika tovuti ya Universe Today kama kitabu cha kielektroniki kwa aina ya PDF inaweza kupakuliwa hapa.  Kwa vile kimeandikwa kwa ajili ya wasomaji wa Marekani muda na mahala pakuangalia matukio hayo hayatakuwa sahihi kwa Tanzania na Afrika Mashariki,

101 Astronomical Events for 2017 by David A. Dickinson

==XX==


Comments