MWEZI MPEVU AJABU Jumatatu Novemba 14


MWEZI MPEVU AJABU


Dr N T Jiwaji

Mwezi mpevu wa Novemba 14 si tu Mwezi mpevu uliokaribu zaidi na Dunia mwaka huu, bali pia ni Mwezi mpevu uliokaribu zaidi katika karne hii ya 21.  Kukaribia zaidi kwa Mwezi mpevu na Dunia katika kipindi cha mwaka mmoja wowote unajulikana kama Mwezi Mpevu Ajabu (SuperMoon) kwa sababu unaonekana mkubwa zaidi kuliko ule unavyoonekana unapokuwa mbali zaidi kutoka Duniani.  Kwa jina la kitaalamu Mwezi Mpevu Ajabu unajulikana kama “perigee-syzygy”.

 

Kila mwaka kuna Mwezi Mpevu Ajabu, lakini huu wa Jumatatu hii ya Novemba 14 ni wa ajabu kwa sababu ni wa karibu zaidi katika miaka 67 iliyopiata tangu 1948, na hautakuwa karibu kiasi hiki tena kwa miaka 18 ijayo hadi Novemba 25, 2034.

 

Kitu chochote kikiwa mbali nasi, huonekana dogo na kikiwa karibu kinaonekana kikubwa. Hali hii hutokea kwa Mwezi pia, kwa vile mzingo wa Mwezi kuizunguka Dunia si duara kamili ila ni umbo la mduaradufu au mduara kama yai.  Kwa hiyo kila mwezi umbali wake na Dunia hubadilika kutoka juu zaidi hadi chini zaidi.  Ukubwa wa Mwezi tunavyouona kutoka hapa Duniani hubadilika kutegemeana na umbali wake kutoka kwetu.

 

Wastani wa umbali kutoka Duniani mpaka kwenye Mwezi ni kilometa laki 380 (380,000km).  Lakini umbali mkubwa zaidi ni kilometa laki 408 (408,000km) na unaitwa “apogee”, wakati umbali wake wa karibu zaidi ni kilometa laki 357 (357,000km) na unaitwa “perigee”. Umbali huu unatofautiana kwa asilimia 15%, kwa hiyo kipenyo cha Mwezi pia utaonekana kuwa mkubwa kwa asilimia hiyo 15%.  Wakati huo huo, eneo lake linaongezeka kwa 30% (yaani mara mbili ya 15%), kwa hiyo Mwezi mpevu wa karibu zaidi utang’aa kwa asilimia 30% zaidi kuliko Mwezi mpevu wa mbali zaidi na Dunia, ambao tunaita KaMwezi Mpevu (MicroMoon).

 

 

Kusema kweli, Mwezi unavutia sana kuuangalia unapochomoza kwenye upeo wa macho au unapotua katika anga za upeo wa upande wa magharibi. Huonekana mkubwa na wenye rangi ya dhahabu kwa vile mwanga wa bluu unakuwa umechujwa na angahewa. Mwezi nusu unaochomoza unavutia sana, utadhani ni bakuli la dhahabu linalonig’inia mbinguni.  Hata Mwezi mpevu unapochomoza angani upande wa mashariki wakati wa machweo huvutia hata zaidi na kung’aa kama sahani kubwa ya njano. Kwa hiyo fikiria jinsi Mwezi Mpevu Ajabu utakavyovutia utapochomoza upeo wa mashariki saa ya magharibi Jumatatu ijayo, Novemba 14.

 

Ingawa umbali wa Mwezi mpevu huu wa Novemba 14 ni wa karibu zaidi, miezi ya kabla na baada ya Novemba nayo pia inahesabiwa kama Miezi Mpevu Ajabu kwa sababu iko ndani ya asilimia 90% ya umbali wa karibu zaidi kwa Mwezi.  Lakini kiastronomia, ukomo wa asilimia 98% hutumikal; ndiyo maana Mwezi mpevu wa Novemba 14 ni Mwezi Mpevu Ajabu hasa wa mwaka 2016 na kitaalamu huitwa “perigee-syzygy”.


 

Umbali wa karibu zaidi wa Mwezi siku ya Novemba 14 utakuwa saa 11.30 jioni, kiasi saa moja kabla ya magharibi ambapo Mwezi mpevu utachomoza kwa madaha katika upeo wa mashariki wakati Jua linazama upande wa magharibi.  Kusema kweli, Novemba 14 ni siku ya ajabu ya kipekee kwa kizazi hiki.  Kwa hiyo tafuta mahali pazuri panapoonekana wazi upeo wa mashariki ili usikose kuuona Mwezi Mpevu Ajabu mwang’avu wa rangi ya njano ukichomoza siku hiyo wakati wa machweo ili uufurahie na pia upate cha kuwajivunia kwa marafiki wako, na kuweza kuwasisimua watoto wako kwa miaka 18 ijayo hadi Mwezi Mpevu Ajabu, yaani “perigee-syzygy” ijayo ya mwaka 2034.


==XX== 

Comments