UTALII WA ANGA ZA USIKU NCHINI TANZANIA

UTALII WA ANGA ZA USIKU NCHINI TANZANIA

Kusoma makala hii kwa Kiingereza bofya hapa

Utalii wa anga ni mwenendo mpya unaofanywa na watalii wa nchi za ulaya magharibi wanaokosa fursa ya kuona nyota kwa uwazi zaidi nchini kwao kutokana na taa na mwanga mkali unatumika katika miji yao. Taa na mwanga huo husababisha anga kuwa angavu zaidi wakati wa usiku na kuficha mwanga hafifu wa nyota. Kwa hiyo ni vigumu sana kuona nyota nyingi sehemu ambapo kuna mwanga mwingi. Mwanga na taa zisio za lazima huchafua mazingira yetu kwa mwanga mwingi mno unaodhuru na kutatanisha binadamu na viumbe vingine. Uchafuzi huu wa mazingira huitwa uchafuzi mwanga (light pollution)

Nchini Tanzania bado kuna maeneo makubwa yenye anga za kiza zaidi kwa sababu maeneo mengi hayana wakazi wengi wa mjini. Hii ni kweli katika Hifadhi za Taifa na maeneo tengefu yanayo hiafadhiwa kwa ajili ya wanyama pori. Bahati nzuri hii inamaanisha kuwa tunahifadhi kiza katika mbuga zetu na hivyo pia kuzilinda dhidi ya uchafuzi mwanga.

Hata katika maeneo makubwa ya mijini kama vile Dar-es-salaam, usiku ni kiza kiasi cha kutuwezesha kuona nyota nyingi angani. Kati ya takribani nyota 3,000 ambazo mtu anaweza kuziona kwenye maeneo ya kiza sana, katika maeneo ya mjini tunaweza kuona kiasi cha nyota angavu sana 300 tu. Hizi zinatosha kukuwezesha kutambua makundi (constellations) maarufu na mawingu-nyota (nebulae).

Ingawa mbingu za kiza zinaweza kuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa kizungu, sisi wenyewe tunaelekea kutojali uzuri wa anga zetu wakati wa usiku. Wakati watalii wa anga huhitaji kwenda mbali sana na kwao, sisi tunaweza kutoka tu nje ya nyumba zetu na kufurahia uzuri wa anga linalotuzunguka.

Si hayo tu. Wakati inakulazimu kufunga safari za mbali kutalii miji mbali mbali Duniani, mbingu zinatufuata pale pale tulipo. Nyota mbinguni zinasogea polepole kiasi kwamba katika usiku mmoja tunaweza kuona mbingu yote inayozunguka Dunia yetu. Hii ni kwa sababu Dunia yetu inazunguka katika mhimili wake kila masaa 24 . Pia, ukiangalia tu anga kwa saa maalum kila siku, kwa mfano saa mili usiku, katika mwaka mmoja utaweza kuona mbingu yote inayotuzunguka. Hii ni kwa sababu mwelekeo wetu wa kuangalia anga hubadilika pole pole kila siku kwa vile Dunia inaizunguka JUA mara moja kila mwaka.

Kwa hiyo badala ya kutumia fedha kwenda kuona sehemu mbalimbali za mbingu, sisi nchini Tanzania tunaweza kutoka nje ya nyumba zetu tu na kuangalia nyota zote mbinguni kwa kuziangalia nyakati mbalimbali za usiku au saa hiyo hiyo ya usiku kwa nyakati tofauti za mwaka. Kwa hiyo ondoka kwenye luninga yako, au klabu za starehe mbali na kinywaji chako, au hata nje ya ofisi yako kwa wale wanaofanya kazi hadi usiku, na toka nje na kuwa mtalii wa anga kwa kuzifanya nyota kukujia. Unacho takiwa ni kuinua kichwa chako kuangalia juu au kulala mkekani ukiangalia mbingu kwa utulivu. Ukitumia darubini utaongeza burudani yako maradufu.

Mwezi huu wa Februari utaona nyota na sayari za kuvutia zifuatazo mbinguni.

MWEZI huonekana kwa uraihisi sana mbinguni. Takribani MWEZI unaonekana vizuri zaidi unapokuwa nusu, yaani kati ya MWEZI mchanga, Februari 22 na MWEZI mpevu Machi 8. Kwa hiyo tarehe zinazofaa zaidi kuangalia MWEZI ni mwishoni mwa Februari.

Mwaka huu Februari ni mwezi wa kipekee kwa sababu, katika nusu ya kwanza ya usiku, unaweza kuona sayari zote zinazoweza kuonekana kwa macho matupu. Siku za mwisho za Februari zitakuwezesha pia kuangalia sayari mbili angavu sana katika anga ya magharibi. Sayari hizo ni ZUHURA (Venus) na SUMBULA (Jupiter) zinazong’ara vikali kuanzia JUA kuchwa kwa JUA hadi saa 3:00 usiku. Kati ya tarehe 25 na 27 Februari, MWEZI Mwandamo utaungana na sayari hizo mbili. Kwa kutumia darubini ya wastani, ZUHURA inaweza kuonekana kama kizio (nusu duara), wakati SUMBULA itaonekana na miezi yake midogo minne na tepe mbili ya mwingu sambamba na ikweta.

Sayari nyingine inanyong’ara sana itakayoonekana mwezi huu ilichomoza upande wa mashariki kabla ya saa 2 usiku na inaonekana usiku kucha ikikatiza anga kuelekea upande wa magharibi kadiri usiku unavyoendelea. Sayari hii ni MIRIHI (Mars) inayong’ara na kuonekana nyekundu. Itang’ara zaidi tarehe 5 Machi wakati itakapochomoza mkabala na JUA linalotua. Mng’aro huu unatokana na mwanga ulioakisiwa kutoka sura ya sayari hiyo ambao tunaona kuwa ni mwanga mwekundu. Kwa kutumia darubini nzuri, utaweza kuona sura yake nyekundu na utandao mweupe wa theluji nchani. Anagani tarehe 7 Machi, MWEZI mpevu utakuwa karibu sana na MIRIHI.

Tarehe 29 Februari ambayo ni siku ya mwisho ya mwezi mrefu, utaona angani sayari nne na MWEZI zimejipanga mbinguni kutoka magharibi kuelekea mashariki. Siku hiyo mara baada ya JUA kuchwa mnamo saa1:00 usiku, angalia Zebaki (Mereury) kwenye upeo wa magharibi, ikiwa na ZUHURA inayong’ara juu yake, kiasi cha nyuzi 30 kutoka kwenye upeo, na kufuatiwa na SUMBULA inayong’ara nyuzi 40 mbinguni na juu yake zaidi utaona nusu MWEZI kwenye mwinuko wa nyuzi 50 juu ya upeo. Zote hizi zimejipanga kwenye mstari unaoitwa njia ya sayari (ecliptic). Ni kwenya njia hii tu ndipo unaweza kuona vitu vyote vilivyo katika Mfumo wa JUA; kama vile MWEZI, JUA na sayari zote, kwa sababu vitu vyote katika Mfumo wa JUA vimepangwa katika bapa moja. Kama unafuata mstari uliyoundwa na ZEBAKI (Mercury), ZUHURA, SUMBULA na MWEZI angani na kuuendeleza hadi upande wa pili, yaani mashariki, utaona kwamba MIRIHI inayachomoza upande wa mashariki pia ipo katika mstari huu huu.

Sayari ya mwisho ya kuweza kuonekana ni ZOHALI (Saturn), inachomoza mnamo saa 4:00 usiku ambao bado ni muda muafaka wa kufurahia kuangalia sayari hii. Kwa vile sayari hii haing’ari sana imejificha kati ya nyota zingine jirani yake. Ukilinganisha mng’aro wa nyota za kawaida zinazomeremeta, mwanga wa sayari haumeremeti. ZOHALI ni sayari ya kufuraisha sana kuiangalia katika darubini kutokana na seti yake ya pete bapa vinavyoizunguka sayari hiyo. Ni miongoni mwa vitu vya kuvutia sana unavyoweza kuviona kwenye darubini.

Mkondo wa Nyota (Miliky Way) linakatiza katikati ya mbingu kutoka kusini-mashariki kuelekea kaskazini-magharibi makundi ya nyota yaliyopo ndani ya njia ya kundi la nyota ni CANIS MAJOR lenye nyota yake kali kuliko zote, iitwayo Sirius, MWINDAJI (ORION) yenye nyota nyingi, NG’OMBE (TAURUS) yenye kundi lake la nyota Hyades na Pleiades; PERSEUS yenye kundi maarufu la mfumo wa nyota liitwalo ANDROMEDA, na mwisho ni kundi lenye umbo la “W” la CASSIOPEIA, lililoko kaskazini. Kinachongezeka mwezi huu ni MSALABA BANDIA (FALSE CROSS), ni umbo linalofanana kwa karibu sana na msalaba wa kusini (Southern Cross), lakini mstari mlalo wake hauelekei kusini. Tafuta kundi la MSALABA BANDIA baada ya saa 3:00 usiku ukichomoza upande wa kusini-mashariki. SIMBO (Leo), inachomoza kichwa chake upande wa mashariki mnamo saa 2:00 usiku na kuweza kutambuliwa kwa urahisi mnamo saa 3:30 usiku.

Nyota tano miongoni mwa nyota angavu sana kumi zinaweza kutambuliwa angani. Ya kwanza kati ya hizo ni, nyota angavu zaidi kuliko zote, Sirius, ikiifuatiwa na Canopus, ambayo ni ya pili kwa kung’ara, inayoonekana upande wa kusini. Rigel imo kwenye kundi la MWINDAJI, na Procyon iko upande wa mashariki. Achernar inatua upande wa magharibi na Betelgeuse iko kwenye kundi la MWINDAJI. Nyota mbili Alpha- na Beta- Centauri, ambozo zinatengeneza mstari chini ya MSALABA WA KUSINI, zitaonekana baada ya saa 4:00 usiku.

Kusoma makala hii kwa Kiingereza bofya hapa