burudaniyasayariangani

Burudani Ya Sayari Angani

FURAHIA BURDANI YA SAYARI

Na Dkt. Noorali Jiwaji

ntjiwaji@yahoo.com

Kuna mabadiliko ya kustaajabisha yanayoendelea kwa wakati huu katika anga ya magharibi mara baada ya jua kuzama yaani wakati wa machweo ya jua. Wakati huo, yaani kama saa kumi na mbili na nusu, sayari mbili zinazong’aa sana, Zuhura (Venus) na Sumbula au kwa jina lingine Mshtarii (Jupiter) zinaonekana kama nyota zinazon’gaa na huwezi kukosa kuziona mara moja.

Chakustaajabisha ni kwamba nyota hizo mbili zinabadilisha kwa dhahiri nafasi zao siku hadi siku, kuanzia sasa hadi mwisho wa mwezi Novemba na kuendelea mwezi Desemba. Kila siku, tazama angani mara baada ya jua kuchwa (mara baada ya magharibi), saa moja kasoro robo hivi, utaona Sayari Zuhura kama nyota inayong’aa sana karibu kabisa na upeo wa macho upande wa magharibi. Sumbula ambayo imefifia kidogo kuliko Zuhura iko nyuzi 15 juu ya Zuhura na zote mbili zimetenganishwa na umbali wa kama upana wa viganja viwili. Sayari hizi mbili zinaonyesha wazi zinavyosogea jinsi siku zinavyopita. Katika kipindi kilichobaki cha mwezi huu Zuhura inasogea juu kuelekea kwa Sumbula na ifikapo mwisho wa mwezi sayari hizo mbili zitakutana kama vito viwili angani.

Fuata picha za anga mara baada ya jua kuchwa (mara baada ya magharibi) uone jinsi sayari hizo mbili zinavoonyesha kubadili nafasi zao za kawaida. Sasa hivi kila moja iko mbali na mwenzake lakini baada ya siku chache, kufikia mwisho wa mwezi Novemba, zitakuwa karibu sana.

Ukweli ni kwamba tarehe moja Desemba, Mwezi nao utajiunga na utaonyesha dhahiri mabadiliko ya nafasi kati yake na sayari hizo mbili saa chache baada ya jua kuzama. Siku hiyo jua litakapozama saa 12:30, jioni mwezi mwandamo utakuwa chini ya jozi hiyo ya sayari, kwa hiyo itaonyesha muonekano wa kupendeza wa Zuhura kwa upande wa kushoto na Sumbula kwa upande wa kulia chini kidogo. Inapofika saa 2:30 usiku mwezi utakuwa kwenye mstari mmoja na sayari hizo mbili zinazong’aa. Hadi ifikapo saa 3 usiku sayari zote tatu zinatua chini ya upeo wa macho kwa upande wa magharibi, mwezi ukiwa juu ya Zuhura na Sumbula.

Hii maana yake nini? Inaonyesha kwamba vitu vilivyoko uwanda wa juu vinasogea. Mabadiliko katika nafasi kati yao yanaonyesha kwamba sayari zenyewe zinasogea, kwa sababu sayari zote zinazunguka jua. Ukweli ni kwamba neno “planet” (sayari) kwa Kigiriki maana yake ni “wazururaji”, yaani kitu ambacho hakitulii mahali pamoja. Wanaastronomia wa kale walifananisha nafasi za sayari na nyota zilizoko karibu nazo na wakagundua kwamba nafasi kati yao zilionyesha dhahiri kubadilika kila baada ya muda fulani.

Walipofananisha nafasi za jozi za nyota waligundua kwamba nyota hazisogeisogei angani na hukaa katika nafasi zao hizo hizo kila wakati. Hivyo maumbo yanayotengenezwa kwa kuunganisha mistari katikati ya nyota yalikuja kutambuliwa kwamba hayabadiliki na maumbo hayo ya makundi ya nyota yanafananishwa na vitu vya kawaida vilivyoko duniani kama wanyama (Simba), ndege (Mwari), wadudu (Nge) binadamu (Mwindaji, Mapacha, Bikira, n.k.).

Tunapoiangalia anga kwa masaa kadhaa au wakati huohuo kwa kipindi cha siku kadhaa utaona kwamba makundi ya nyota yanaonekana pande mbalimbali na nyakati mbalimbali katika mwaka. Lakini maumbo ya makundi ya nyota yanabaki hivyo hivyo. Kwa hiyo tuna uhakika kwamba nyota hazisogeisogei (ingawa kwa kweli zinasogea pole pole mno na zitachukuwa kwa maelfu ya miaka kuonyesha mabadiliko).

Kwa hiyo kusogea kokote kwa nyota kunahusishwa na na sayari na Mwezi. Sayari zinapozunguka jua, mwenendo wao angani unaonekana kwamba unatoka magharibi kwenda mashariki. Katika mwenendo wa sayari ambao tunaouona upande wa magharibi wakati huu, Zuhura inasogea juu kufikia Sumbula kwa vile Zuhura ina mwendo wa kasi kuzunguka jua, wakati Sumbula haionekani kusogea kabisa kwa kuwa sayari hii iko mbali sana nasi. Kwa kuwa Zuhura iko karibu sana na dunia kusogea kwake unaonekana dhahiri na inapanda juu na kukutana na Sumbula tarehe moja Desemba.

Mabadiliko katika nafasi ya mwezi siku hiyo ya Desemba moja pia yanasababishwa na kusogea kwa mwezi. Kwa kuwa mwezi uko karibu na sisi kuliko Zuhura, kusogea kwake angani kunaonekanka zaidi, na hata ndani ya masaa machache unaweza kutambua msogeo huo.

Ukitumia darubini kuangalia Zuhura utawezakuona umbo la mstatili. Hii ni kwa sababu sehemu yake iko katika giza la usiku huko. Jinsi miezi inavyopita umbo la Zuhura kwenye darubini utaona unabadilika sana. Hii inatokana na mzunguko wake kuizunguka Jua. Ikiwa mbali na Dunia, inaonekana kama kisahani cha mviringo. Inapokuwa umbali wa kiasi sura yake inayoonekana ukiwa Duniani inabadilike kuwa nusu kisahani katikati ya mzunguko wake. Inaonekana nusu kwa kuwa nusu yake iko upande wa mchana na nusu iko upande wa usiku. Hii ni sawa na wakati mwezi unapokuwa na umbo la nusu mwezi, na kwa sababu hiyo hiyo: inamulikwa na jua upande mmoja ambao unasababisha Zuhura kuonekana kama nusu mwezi. Baada ya hape sura yake itakuwa ya mwezi mwandamo kwa vile Zuhura itaendelea kukaribia zaidi Dunia.

Ifikapo Machi 10 mwakani, Zuhura itavutia sana kwa umbo na ukubwa kama ukiiangalia kwa darubini. Umbo lake litabadilika kuwa la mwezi mwandamo na kuwa na ukubwa mara tatu. Katika kipindi hicho Zuhura inaendelea kung’aa kwa kuwa kupungua kwa eneo lake linalopata mwanga kunafidiwa kuongezeka kwa ukubwa wake kwa ajili ya kutukaribia zaidi.

Kwa taarifa zaidi kuhusu yanayotokea angani mwezi huu tembelea tovuti yetu: www.astronomy2009.ac.tz kwa makala kamili na taarifa muhimu hukusu elimu ya nyota (Astronomia) hapa Tanzania na kuhusu Mwaka wa Kimataifa wa Astronomia 2009 ambao utaadhimishwa kuanzia Januari. (ntjiwaji@yahoo.com)

MWISHO