MPITO WA SAYARI YA ZUHURA JUANI

MPITO WA SAYARI YA ZUHURA JUANI

MUONEKANO WA MPITO WA ZUHURA DUNIANI

Mwishoni mwa wiki ya kwanza ya mwezi Juni mwaka huu, tukio la nadra sana kuonekana kiastronomi litaonekana nchini Tanzania tarehe 6 Juni. Tukio hili ni kupita kwa sayari ya Zuhura kwenye sura ya Jua. Tukio hili halitokei tena hadi baada ya miaka mingine 105, kwa hiyo hakuna binadamu yeyote anayeishi leo, atakayekuwa hai wakati huo.

Kihistoria, tukio hili pia lilionyesha mbinu ya kwanza ya moja kwa moja ya kupima umbali wa Dunia kutoka kwenye Jua (Astronomical Unit – AU). Umbali huu ni kipimo cha msingi kinachotumika kupima umbali na ukubwa wa mfumo wetu Jua na sayari zinazolizunguka. Kwa hiyo si vigumu kutambua umuhimu wa tukio litakalotokea siku chache tu zijazo hapo Juni 6, 2012.

Jua liko mbali kabisa kufikiwa na binadamu kwa uwezekano wowote wa kupima moja kwa moja umbali wa Dunia kutoka kwenye Jua. Mwaka 1631, Johannes Kepler alieleza kuwa nyota angavu sana ya asubuhi na jioni, yaani Zuhura, ambayo ni sayari yenye mzingo wa ndani ya ule wa Dunia, inaweza kutoa mbinu ya kupimia umbali huu wa msingi wa kiastronomia (AU), kila mara Zuhura inapokuwa katika mstari sawia kati ya Dunia na Jua.

Zingatia kwamba kama Mwezi ungekuwa kati ya Dunia na Jua, ungezuia Jua kabisa na kungetokea kupatwa kwa jua. Kwa vile Zuhura iko mbali sana, inaonekana kama kitone kidogo sana mbinguni. Kwa hiyo ingawa haiwezi kabisa kuzuia Jua, bado ni hali ya kupatwa.

Mbinu inayotumika kupima umbali wa Dunia kutoka Jua wakati wa Mpito wa Zuhura inatumia tofauti ya nafasi dhahiri ya kitu kinapoangaliwa kutoka mahali tofauti. Hii inajulikana kama “paralexi”(parallax) na ni vile mtu anavyokiona kitu cha karibu kinapolinganishwa na vitu vya mbali sana kwa mfano anga au milima. Mtazamaji anavyo endelea mbele, ndivyo kitu cha karibu husogea nyuma. Kwa mafano, tunapoangalia vitu vya karibu kama miti kutoka kwenye dirisha la gari au basi linalotembea kwa kasi, miti ya karibu huonekana kusogea nyuma haraka dhidi ya anga iliyo mbali.

Wakati wa hali ya kupatwa na Zuhura, paralexi husababisha kidoti cha Zuhura kuonekana kikiwa mahali tofauti kwenye mandhari ya Jua liapongaliwa kutoka mahali tofauti Duniani. Ukifananisha hali hii na mfano wetu wa miti na basi, Zuhura (miti) inabadili nafazi dhidi ya mandhari ya Jua (mbingu) inapoangaliwa kutoka kwenye sehemu tofauti za Dunia (kusogea mbele kutokana na mwendo wa gari au basi).

Kupita kwa Zuhura kulianza kutumiwa na mwanasayansi shupavu, kijana Jeremiah Horrocks, aliyetabiri na kuangalia Mpito wa Zuhura wa mwaka 1639 na kukokotoa umbali wa Dunia kutoka Jua kama ni kilomita milioni 96 (bahati mbaya sana kwa sayansi, Jeremiah alifariki akiwa na umri wa miaka 22 tu). Kipimo hiki kilikuwa pungufu kwa zaidi ya kilomita milioni 50, lakini kilitoa changamoto ya kujaribu kupata umbali sahihi zaidi wakati wa Mpito wa Zuhura mwaka 1761-69. Edmund Halley (wa umaarufu wa kimondo cha Halley) alikuwa wa kwanza kupendekeza matumizi ya mbinu ya paralexi wakati wa Mpito wa Zuhura. Utafiti huu umesababisha kipimo sahihi zaidi cha kilomita milioni 153 kwa umbali wa Dunia kutoka Jua (AU).

Hata hivyo kosa linalotokana na “athari ya muono wa nyuma” (backdrop effect) katika kidoti cha Zuhura inayounganisha mapema mno kidoti cheusi cha Zuhura na ukingo wa duara la Jua, limesababisha upungufu katika kipimo kilichokokotolewa.

Uvumbuzi huu uliamsha juhudi zaidi za kimataifa kushirikiana kufanya vipimo sahihi zaidi wakati wa matukio ya Mipito ya yaliofuata 1874-82. Matokeo yake ni kupata kipimo cha kuaminika zaidi cha kilomita milioni 149.50 kwa umbali kutoka Dunia – Jua (AU).

Kwa hiyo Mpito wa Zuhura ulitoa nafasi ya kufanya mfululizo wa majaribio ya kisayansi yaliyoendelea pole pole kwa zaidi ya miaka 300 katika maeneo mbalimbali Duniani na kupata kipimo cha kuaminika zaidi cha umbali wa Dunia kutoka Jua (AU). Imeonyesha namna maarifa ya nadharia thabiti ya Newton na Kepler, yaliyotumiwa na wanasayansi kufanya majaribio yenye uvumilivu kwa karne nyingi katika shauku yao kubwa ya kupata vipimo vya kuaminika. Bila shaka ulikuwa ushindi wa mchakato wa kisayansi uliosababisha uvumbuzi, na hatimaye maendeleo kwa binadamu.

Maendeleo katika maeneo mengine ya sayansi kama vile rada, yamewezesha vipimo sahihi vya umbali wa sayari za karibu. Kwa hiyo umbali wa Jua sasa unaweza kukokotolewa kwa usahihi zaidi bila ya kutumia Mpito wa Zuhura. Hivyo tukio la hivi sasa la tarehe 6 Juni, 2012 linatoa nafasi nzuri ya elimu kwa vitendo na kutoa changamoto kwa akili za wanasayansi vijana na kutoa mtazamo wa kihistoria wa maendeleo ya sayansi kwa ushirikiano wa kimataifa. Katika enzi hii ya mtandao wa Intaneti, ushirikiano huo ni rahisi sana hata kwa wanasayansi wanaoibuka mashuleni.

Matumizi mengine muhimu ya tukio hili la Mpito wa Zuhura ni kupima mbinu na vifaa vya kutafuta sayari zingine zinazozunguka nyota zilizo mbali. Mbinu hii inahusisha kupima mabadiliko ya ung’avu wa nyota wakati sayari inapokuwa mbele yake. Hali hii itakuwa sawa na itakavyotokea wakati Zuhura itakapokuwa mbele ya Jua, tarehe 6 Juni, 2012.

Kupungua kwa ung’avu wa nyota (au Jua) ni kidogo sana. Je unaweza kufikiria kiasi cha mabadiliko ya ung’avu utakaoweza kuuona katika mwanga wa taa za mbele za gari wakati nzi atakapokuwa mbele yake? Wakati wa kupita Zuhura , tarehe 6 Juni, wanasayansi wataona kama vifaa vyao vinaweza kuonyesha kupungua kokote kwa ung’avu mkubwa wa Jua kutokana na kidoti kidogo cha Zuhura kikiwa mbele yake.

Alfajiri ya tarehe 6 Juni, sisi tulioko Tanzania tutashuhudia mwisho wa tukio la Mpito wa Zuhura kuanzia jua kupambazuka (mawio) saa 12:34 hadi saa 1:49 asubuhi. Wakati wa mawio kidoti kidogo cha Zuhura kitakuwa karibu sana na ulingo wa juu wa kushoto wa Jua, kikijiandaa kuondoka kwenye uso mng’avu wa Jua. Utahitaji miwani maalum ya Kupatwa ili uone tukio hili, kwa kuwa Jua ni ng’avu sana na macho yako yanaweza kupofuka kama utalazimisha macho yako kuendelea kuliangalia.

Wakati unapoangalia kidoti kidogo kupitia miwani maalum ya kupatwa kuanzia mawio au kupambazuka tarehe 6 Juni, utaona kitone kidogo cha Zuhura kikisogea pole pole kuelekea ukingo wa Jua na mwishoni kuondoka katika sura ya Jua, ambapo itakuwa mwisho wa Mpito.

Usipokuwa na miwani maalum ya kuangalia Jua, unaweza kuona Mpito wa Zuhura kwa kupitisha mwanga we Jua katika tundu dogo katika karatasi kubwa. Utaona sura ya Jua upande wa pili ya karatasi ukiielekeza ukutani au sakafuni.

Ukilinganisha saa yako na saa ya kimataifa inayopatikana kwa mfano katika tovuti ya http://tycho.usno.navy.mil/simpletime.html unaweza kupima muda wa kidoti kinapounganika kwanza na ukingo wa Jua na muda wa kuacha ukingo wa Jua. Unaweza kupeleka muda hizi ulizopima kwenya mkusanyo wa data, kwa mfano katika tovuti, http://www.venus2012.de/php/datacontacttimes.php

Mstari sawia wa mpangilio wa Dunia-Zuhura-Jua hutokea nadra sana. Tukio hili hutokea mara moja kwa kila karne. Lakini linapotokea, kufanya hivyo kwa jozi. Mpito wa Zuhura wa mwisho ulikuwa mwaka 2004 na Mpito wa pili katika jozi hii ni ule tunaosubiri kuuona alfajiri ya Jumatano, tarehe 6 Juni, 2012. Mpito mwingine wa Zuhura hakutatokea mpaka baada ya miaka 105 yaani mwaka 2117. Kwa hiyo hii ni fursa ya pekee maishani kuona tukio la nadra kabisa la kiastronomia na kufurahia umuhimu wake wa kihistoria na wa kisayansi. Kwa maelezo zaidi fungua tovuti www.astronomyitanzania.or.tz

MWISHO