Mwezi Kupatwa Jumamosi

Mwezi Kupatwa Jumamosi

Dkt. N T Jiwaji

ntjiwaji@yahoo.com

Kupatwa kwa Mwezi ni tukio linaloweza kutazamwa kutoka sehemu kubwa ya dunia na linaweza kushuhudiwa kwa wakati mmoja na mamilioni ya watu muda ule ule wakati tukio linapotokea angani. Kwa hiyo tukio hili linachukuliwa kama ni la kawaida na kuchukuliwa kama tunavyochukulia kuchomoza kwa Mwezi. Kwa upande mwingine, kupatwa kabisa kwa Jua huaonekana katika ukanda mwembamba tu wenye upana wa kiasi cha kilomita 100 hivi. Hivyo idadi ndogo sana ya watu wamewahi kuona Jua likipatwa kabisa na kuwa kiza kama usiku pamoja na anga ya moto inayozunguka Jua.

Tukio la kupatwa kwa Mwezi litakalotokea Jumamosi hii, tarehe 10 Desemba. Ni tukio muhimu kwa nchi yetu kwa vile ni mwanzo wa kipindi kingine cha miaka 50 ya uhuru wetu. Pamoja na hiyo, tukio Jumamosi hii litashuhudiwa na watu wachache sana duniani. Mwezi utaonekana umepatwa kabisa katika bara la Asia tu. Hapa Tanzania Jumamosi hii, sisi tutaona mwisho tu wa kupatwa kwa Mwezi. Wakati wa magharibi, wakati Jua likizama, ukiangalia upande wa mashariki utaona Mwezi Mpevu ukichomoza, na nusu ya sura ya Mwezi itakuwa imefunikwa na kivuli kizito cha Dunia.

Baada ya tukio la mwisho la kupatwa kabisa kwa Mwezi lililotokea tarehe 15 Juni mwaka huu na kuficha kabisa sura ya Mwezi, kupatwa tarehe 10 Desemba itatokea upeoni na nusu tu ya sura itafichwa. Pia kutakuwa na tofauti kubwa katika kiasi cha kupatwa kitakachoonekana sehemu mbalimbali za Tanzania. Wale wanaoishi upande wa mashariki wa nchi wataona sehemu kubwa ya kupatwa huko kuliko itakavyoonekana upande wa magharibi mwa nchi.

Katika kanda ya pwani, Mwezi Mpevu utachomoza saa 12:33 jioni baada ya Jua kuchwa saa 12:27 jioni. Wakati huu, nusu ya juu-kushoto ya Mwezi itakuwa imefunikwa na kivuli cha Dunia. Mwezi utaendelea kupanda wakati kivuli nacho kinapotea polepole. Kupatwa kutakapokwisha saa 1:18 usiku, Mwezi utakuwa umepanda kiasi cha nyuzi/digrii 10, kwa hiyo watu wengi wa ukanda wa mashariki wataweza kuona kupatwa huko alimradi upeo wa mashariki usiwe na mawingu au kipingamizi kingine. Ikiwezekana, chagua mahali ambapo upeo wa mashariki unakuwa wazi kabisa, kwa mfano sehemu ya pwani, na utakuwa miongoni mwa watu wachache watakaobahatika kuangalia tukio hili adimu.

Upande wa magharibi mwa Tanzania, kwa mfano pale Kigoma, Mwezi utachomoza saa 1:07 usiku wakati kupatwa kunakaribia mwisho, na sehemu ndogo sana ya ukingo wa juu-kushoto mwa Mwezi utakuwaumefunikwa na kivuli kilichofunika. Kukosekana kwa bahari upande wa mashariki sehemu hizo, mtu itamlazimu kutafuta sehemu ya upeo tambarare zaidi ili aweze kuona sehemu ya mwisho ya kupatwa huko.

Kupatwa hutokea wakati Jua, Dunia na Mwezi vimejipanga mstari mmoja kiasi kwamba kivuli cha kimojawapo kinaweza kuangukia kingine. Kupatwa kwa Jua hutokea wakati kivuli kidogo cha Mwezi kinapoangukia kwenye sehemu ndogo tu ya Dunia. Kupatwa kwa Mwezi hutokea wakati kivuli kikubwa cha Dunia kinafunika Mwezi wetu mdogo. Wakati wa kupatwa kabisa, Mwezi wote unamezwa na kivuli cha Dunia. Kama sehemu ya Mwezi inabaki nje ya kivuli huwa tunasema ni kupatwa kwa sehemu ya Mwezi, na ndicho tunachokiona hapa Tanzania siku ya Jumamosi tarehe 10 Desemba wakati wa Jua kuchwa.

Wakati ukiangalia tukio la kupatawa kwa Mwezi, tafakari hali ilivyo hapo juu angani. Kwa vile Jua liko upande wa magharibi na limezama tu baada ya kuchwa, na Dunia ndipo uliposimama, na Mwezi unajichomoza juu ya upeo upande wa mashariki, basi utaweza kuamini kuwa mwanga wa Jua ndiyo umezuiliwa na Dunia na kivuli cha Dunia ndicho kimeangukia Mwezini.

Fuata mchoro wa mundo wa kupatwa ka Mwezi (shukrani kwa Fred Espenak, www.MrEclipse.com) wakati unatafakari tukio hili na utaelewa jinsi Jua, Dunia na Mwezi zimepangika angani katika mstari ulionyooka. Wakati kupatwa kwa Mwezi kunaendelea, waza kwamba kivuli cha Dunia kinatoweka pole pole kutoka kwenye sura ya Mwezi, na utaelewa kuwa umeshuhudia tukio linalotokea mbali sana Mwezini, karibu kilometa nusu milioni kutoka kwetu. Kwa kawaida, mara moja kila mwezi, siku ya Mwezi Mpevu pia Jua, Dunia na Mwezi zinakuja kuwa katika mstari mmoja lakini ni mstari ambao haukunyooka moja kwa moja. Kwa hiyo nuru ya Jua huwasha sura nzima ya Mwezi na kutuwezesha kuona Mwezi Mpevu kila mwezi.

Usisahau pia kuangalia sayari mbili zinazong’aa kama taa kali. Upande wa magharibi, utaona sayari ya Zuhura na kwa upande wa mashariki utaona sayari ya Sambulaa. Sayari zote mbili hizi tutaendelea kuziona kwa miezi kadhaa ijayo.