Mabadiliko katika Mwonekano wa Zuhura Angani

Mabadiliko katika Mwonekano wa Zuhura Angani

Katika miezi kadhaa ijayo hadi mwakani, kila baada ya Jua kuchwa ukiinua kichwa juu kidogo tu, upande wa magharibi na mashariki utashuhudia sayari mbili za kusisimua zinazongara sana. Sayari hizo mbili zinaonekana kama nyota kali kwenye mbingu za mashariki na magharibi ni sayari za Zuhura (Venus) na Sumbula (Jupiter). Zuhura inajiandaa kutuonyesha mandhari ya kuvutia katika kipindi cha miezi mingi ijayo hadi mwezi Mei mwakani.

Kwa sasa Zuhura iko kwenye mbingu ya magharibi mara tu Jua linapokuchwa na inapanda kadri siku zinavyopita. Wakati huo huo, Sumbula nayo inachomoza upande wa mashariki. Sayari zote mbili zitakwenda juu zaidi mbinguni kadri siku zinavyopita.

Tofauti kati yao ni namna nafasi zao zinavyobadilika baada ya saa za kuchwa Jua. Zuhura inazama upeoni upande wa magharibi jinsi masaa yanavyopita, wakati Sumbula inapanda juu upande wa mashariki, kadri Dunia inavyozunguka katika muhimili wake.

Pamoja na hiyo, nafasi za sayari mbili hizo zitabadilika siku hadi siku ukiziangalia wakati ule ule kila siku kwa siku nyingi. Mabadiliko hayo yanategemea mzingo (orbit) wa Dunia kuizunguka Jua. Kadri siku zinavyopita, tunaweza kuona nyota mbali mbali mpya angani usiku kwa sababu tunaona ulimwengu kutoka mielekeo inayobadilika daima. Kwa kuwa Sumbula ni sayari iliyoko mbali sana (zaidi ya mara tano ya umbali kutoka kwenye Jua ililinganishwa na Dunia) na inazunguka pole pole sana kwenye mzingo wake (huchukua takribani miaka 12 kukamilisha mzingo mmoja), huonekana angani katika nafasi ile ile. Kwa hiyo, wakati Dunia inapobadilisha nafazi yake kwenye mzinga, Sambula itaonekana juu zaidi na zaidi kila Jua linapokuchwa, na kuwa juu kabisa (utosini) mwishoni mwa mwaka,

Kwa upande wa Zuhura, hali ni tofauti kabisa. Kwanza sayari hii iko umbali war robo tatu kutoka kwenye Jua ililinganishwa na Dunia. Kwa hiyo mzingo wake umo ndani ya mzingo wa Dunia. Wakati mwingine sayari ya Zuhura inakuja karibu zaidi na Dunia wakati zinakuwa upande mmoja na Jua (hujurikana kama “muunganiko wa kiwango cha chini”).

Zuhura ikiwa upande wa pili wa Jua kutoka Dunia (yaani katika “muunganiko wa kiwango cha juu”), Zuhura inakuwa mbali zaidi (takribani umbali wa mara sita), kutoka katika Dunia. Pia, Zuhura inakwenda kwa kasi zaidi kwenye mzingo wake ina tumia siku 225 tu kuizunguka Jua (yaani theluthi mbili ya mwaka mmoja). Kwa hiyo hupita Dunia kila baada ya siku 584. Hii husababisha mahali pa Zuhura angani saa ya jioni kubadilika siku hadi siku.

Kwa kuwa mzingo wa Zuhura umo ndani ya ule wa Dunia haiwezi kamwe kuonekana utosini nyakati za usiku. Mwinuko wa juu zaidi inayoweza kuonekana Zuhura wakati Jua linapokuchwa ni nyuzi 47.

Ingawa ukubwa wa sayari ya Zuhura ni karibu sawa na ukubwa wa Dunia, kutokana na umbali wake kutoka kwetu muono wa ukubwa wake halisi (kama unavyoonekana kupitia kwenye darubini) unabadilika takribani mara sita kati ya umbali zaidi na ukaribu na Dunia.

Matokeo mengine ya mzingo wa Zuhura kuwa ndani ya Dunia yetu ni kwamba Zuhura inaonyesha mabadiliko ya sura yake sawa na mabadiliko unayoona kwenye umbo la Mwezi wetu. Kusema kweli, kama mtu hakuwa makini anaweza kudanganyika kwa kufikiria kuwa hilali ya Zuhura unayoona kwenye darubini ni hilali ya Mwezi.

Mwonekano wa mabadiliko wa Zuhura katika kipindi cha miezi saba ijayo umeonyeshwa kwenye mchoro pamoja na sura mbali mbali za sayari hiyo kwenye tarehe tofauti. Safari ya Zuhura kwenye mbingu za magharibi ilianza chini kwenye upeo wa magharibi mwezi Oktoba. Wakati huo Zuhura ilikuwa kwenye “muunganiko wa kiwango cha juu” na Dunia. Mwezi wa Novemba, njia yake angani magharibi itaelekea kushoto na kuwa juu zaidi kila usiku. Wakati huu ikiangaliwa kwa darubini itaonekana ndogo sana kama nukta ya duara.

Katika hatua inayofuata ya mwendo wa Zuhura mwezi wa Desemba na Januari mwakani itabadilisha mwelekeo kwenda kulia katika anga ya magharibi, na kuinuka angani hadi nyuzi 35 wakati wa Jua kuchwa. Sura yake katika hatua hii inajulikana kuwa sura ya kuelekea Mwezi mpevu, na kuonekana kwenye darubini kama nukta kubwa yenye ulingo mmoja uliokatwa.

Kuanzia Februari hadi Aprili 2012 itakenda kwa kasi sana kwa na kubaki katika mwinuko ule ule wa kiasi cha nyuzi 35. Katika darubini itaonekana kubwa kidogo lakini sura yake itakuwa nusu mduara.

Katika mwezi wa Mei itaanza kuzama zaidi na zaidi upande wa magharibi na ukubwa wake halisi kuongezeka kwa zaidi ya mara tano kuliko ilipoanza safari yake ya mwezi Oktoba. Kupitia darubini sura ya Zuhura itaonekana kama hilali ndogo. Ingawa hilali itakuwa nyembamba zaidi, sayari hiyo itang’ara kwa nuru ile ile kwa vile ukubwa wake unaongezeka kadri inavyokaribia Dunia.

Sayari itakaribia Jua upeoni mwisho wa Mei na baada ya hapo itatoweka chini ya upeo wakati Jua linapotua. Cha kuzingatia ni kwamba wakati huu Zuhura itakuwa inaelekea kukutana na Jua tarehe 6 Juni 2012, wakati itakapovuka uso wa Jua. Kisanyansi hali hii hujulikana kama “Mpito wa Zuhura Juani” (Transit of Venus), tukio ambalo halitarudia maishani kwetu kwa sababu itapita tena zaidi ya karne moja hadi mwaka 2117. Hapa Tanzania, tutaweza kuona “Mpito wa Zuhura Juani” wakati Jua litakapopambazuka tarehe 6 Juni,

Wakati wa kusafiri kwa Zuhura katika mbingu ya magharibi katika kipindi cha miezi saba kutakuwa na kukutana kwa karibu na sayari, nyota na Mwezi.

Tangu mwanzo wa mwezi huu sayari nyingine ya mzingo wa ndani, yaani Zebaki (Mercury), ambayo ni sayari ndogo sana na iliyokaribu na Jua, imeisogelea sana sayari ya Zuhura. Siku ya Jumapili tarehe 6 Novemba sayari mbili hizo zilikuwa karibu sana zikionekana katika usawa unaolingana, na kutengana kwa upana wa kidole kimoja tu.

Kwa wakati huu Sayari mbili hizo ziko kwenye kundi la nyota iitwayo Nge (Scorpion) na zinaisogelea kwa karibu sana nyota kubwa nyekundu ya Antares. Tarehe 10 Novemba Zuhura, Zebaki na Antres zitaunganika kwa karibu sana na kuonyesha mwonekano wa kuvutia sana.

Baada ya hapo, Zuhura itakuwa imeacha chini Zebaki na kuendelea kupanda mbinguni. Mwisho wa Novemba na mwanzo wa Desemba, Zuhura itakuwa imehama kutoka kwenye Nge na kwenda kwenye kundi la nyota la Mshale (Sagittarius), msogeo wa takribani nyuzi 30 kwenye mbingu ya jioni. Kwakuona tofauti hiyo utakuwa umeshuhudia mwendo halisi wa sayari mbinguni.

Tarehe 26 Novemba, Zebaki na Zuhura zitafuatwa na hilali ndogo ya Mwezi Mwandamo na akuwa kati ya sayari hizo mbili. Huu utakuwa mwonekano wa kuvutia kuangalia kwenye mbingu za magharibi wakati wa jioni. Usikose kuangalia. Siku inayofuata, kioja kinaendelea wakati hilali ndogo ya Mwezi itakuwa bado juu mbinguni, na Zuhura na Zebaki zikiwa chini yake.

Zebaki ikiwa sayari ya ndani yenye mzingo wa ndani ya Dunia kama ilivyo Zuhura, nayo inaonyesha mabadiliko ya sura kama ukiiona katika darubini. Kuanzia tarehe 10 Novemba hadi mwisho wa Novemba, Zebaki itaonekana kuwa chini na chini zaidi kwenye anga ya magharibi na sura yake itabadilika kutoka nusu hadi itakuwa hilali. Hii ni fursa nzuri kwa wale wenye darubini kuangalia sayari inayobadilika haraka na kuangalia sura za hilali, hali ambayo ni adimu sana kuona.

Katika kipindi cha miezi ijayo utasoma taarifa fupi fupi kuhusu matukio mengine na mionekano ya matukio ambayo Zuhura itatushangaza. Kwa hiyo endelea kuwa hamu nashauku ya kufuatilia anga za usiku hapa Tanzania.