mwaka2009niwaastronomia

Mwaka 2009 ni wa ASTRONOMIA

Mwaka 2009 ni wa ASTRONOMIA

Imeandikwa na Beniel R Seka

sekabeniel AT yahoo DOT com

Mwaka 2009 ni mwaka wa kimataifa wa Astronomia au kwa Kiingereza International Year of Astronomy (IYA). Azimio hilo la kuwa na mwaka wa unajimu umepitishwa na Umoja wa Mataifa tarehe 20 Desemba, 2007 baada ya kupendekezwa na ‘The International Astronomical Union’ na kuungwa mkono na UNESCO kwa ajili ya kuwasaidia wanadamu kugundua upya nafasi yao katika ulimwengu kwa kupitia anga na hatimaye kujiweka katika wazo la binafsi la kujua maajabu na ugunduzi. Mwaka 2009 utakuwa miaka 400 tangu Mwanasayansi, Galileo Gallilei alipogundua darubini.

Baadhi ya shughuli zitakazofanyika kimataifa ni kuwapatia walimu uwezo kwa kujenga mpango utakaoitwa Galileo Teacher Teacher-Training Programme (GTTP). Mpango huo umekusudiwa kutengeneza mtandao wa kimataifa wa ‘Mabalozi wa Galileo’ waliobobea ifikapo 2012. Mabalozi hawa watawafunza ‘walimu mabingwa wa Galileo’ katika kutumia na kufikisha Elimu ya unajimu na rasilimali zake darasani ndani ya mtaala wa sayansi.

Galileo ni nani? Historia ya mnajimu Galileo Galilei ina weza kupatikana katika vitabu kadhaa vya wagunduzi na vya Historia. Katika kitabu cha Mfumo wa Jua kilichochapishw na Mture Educational Publishers, tunasoma kuwa Galileo Galilei aliishi 1564 hadi 1642. Mwanasyansi huyu kutoka Italia baada ya kutumia darubini aliweza kuuthibitishia Ulimwengu kwamba dunia ndiyo inayoizunguka dunia tamko ambalo lilimsababishia matatizo kwa kanisa lake ambalo lilishikili imani kwamba Dunia iko katikati na syari, nyota na mwezi huizunguka. Wazo la kanisa lilikuwa linaendeleza fikra za mwanasayansi Mgiriki wa karne ya pili, Claudius Ptolomy. Hata hivyo mwanasayansi wa Poland aliyeishi mwaka 1473 hadi mwaka 1543 aliamini kuwa Dunia hulizunguka Jua lakini hakuweza kufanya wazo lake likubalike. Baada ya ugunduzi wa Galileo Galilei, wazo hilo lilikubalika hadi leo.

Ugunduzi wa darubini uliwezesha wanasayansi kujua mambo mengi zaidi kuhusu mfumo wa Jua (The Solar System). Kwa mfano, Johannes Kepler aliyeishi mwaka 1571 hadi mwaka 1630, alieleza kuwa obiti za sayari ni duaradufu na si duara kama wengi walivykuwa wakiamini. Galileo Galilei katika mwaka 1610 aliweza kugundua miezi mine kati ya miezi kumi na sita inayoizunguka sayari ya Jupita au Sumbula kama wengine wanavyoiita. Sayari ya mbali, Yuranusi au Zohari kama wengine walivyozoea kuiita, iliyoko umbali upatao kilometa bilioni mbili nukta nane (km 2 800 000 000) iligunduliwa na Mwingereza William Herschel mwaka 1781. Mwaka 1846, Urbain Leverrier na mwenzake John Coach Adams , waligundua sayari ya Neptuni au Kauri, sayari ya nane kutoka Jua. Wanasayansi hao walikuwa wanatafuta sayari ambayo kani yake ilikuwa inaathiri mwondoko wa sayari ya Yuranusi. Hatimaye sayari ya tisa kutoka Jua, Pluto au Utaridi, iligunduliwa mwaka1930 wakat wanasayansi walipokuwa wanachunguza ang za juu kwa darubini zenye uwezo mkubwa.

Darubini hazikusaidia kujua zaidi mabo ya sayari tu. Zilisaidia pia kugundua msururu wa astroidi kati ya Jupita na Maazi (Mihiri). Hizo astroidi ambzo zinaweza kufikiriwa kama visayari vidogo ni miamba iliyomegeka kwenye sayari. Miamba hiyo imeweza kutambuliwa na kupewa majina. Astroidi kubwa kuliko zote inaitwa Ceres. Nyingine ni Vesta, Davida, Doris, Pals, Juno, Adonis, Icarus na Hidlgo. Inasemekana baadhi ya astroidi hutoka kwenye obiti zake ambacho ni kitendo hatari sana kwa dunia yetu. Mwaka1989 astroidi moja iliikosakosa Dunia ilipopita kilomita 1 120 000 karibu nayo. Ingepita saa chche baada, ingeigonga Dunia na hakuna liyejua inakuja. Ilikuwa na kipenyo cha kilomita moja.

Kitu kingine kinachotokea angani mara kadhaa ni kometi au nyotamkia. Darubini ni muhimu kwa kuangalia kometi. Kometi inayojulikana sana ni ile ya Halley ambaye Halley aliigundua mwaka 1682. Kometi hiyo huonekana kila miaka 76. Mara ya mwasho kometi hiyo ilionekana mwaka 1986. Kometi iliyogunduliwa siku za karibuni inaitwa Hale-Bopp tarehe 22 Julai, 1995, wagunduzi wake wakiwa ni Alan Hale na Tom Bopp, wote wawili raia wa Amerika. Mwaka 1997, kometi hiyo ilikuwa bado ipo kwenye anga yetu.

IAU imekupatia anwani pepe yake ambayo ni iya2009 AT eso DOT org au Kwa Tanzania tunaye mratibu, Dr Noorali Jiwaji ntjiwaji AT yahoo DOT com; noorali DOT jiwaji AT out DOT ac DOT tz. Mwandishi wa makala ni mkuza mitaala Taasisi ya Elimu Tanzania sekabeniel AT yahoo DOT com .