SAYARI ZA KUTANA ANGANI

SAYARI ZA KUTANA ANGANI

Dkt. N T. Jiwaji

Sayari mbili zinazong’aa vikali, Zuhura (Venus) na Sambula (Jupiter) zilizokuwa zikionekana angani tangu Novemba mwaka jana, sasa ziko jirani katika anga za Magharibi saa za jioni ya saa moja. Sayari zote mbili zinang’aa mno ila Zuhura inang’aa zaidi.

Sayari hizo mbili zitaonekana jirani kabisa jioni ya Alhamisi Machi 15. Sambula, iendayo polepole sana, itaipita Zuhura baada ya Jumamosi Machi 16 ambapo zitakuwa sawia. Kuwa jirani angani ni muono wetu tu tunavyoziona. Sayari zenyewe zimepishana angani kwa mamilioni ya kilomita. Baada ya Machi 16 Sambula itaonekana chini ya Zuhura inavyooneshwa katika picha.

Hali hii ya kuwa jirani hutokea nadra sana. Tukio la kusisimua kama hili halitatokea tena hadi July 2015 ambapo sayari hizi mbili zitakuwa jirani zaidi kwa mara tano ya zilivyo sasa hivi.

Jioni ya tarehe 25 na 26 Machi, Mwezi hilali mwembamba utaunganika na sayari hizi mbili na kutoa mandhari ya kuvutia mno katika anga za jioni.

Kati ya sayari nane (siyo tisa!) katika Mfumo wetu wa Jua, sita kati yao huonekana kwa macho bila kutumia darubini. Kwa wakati huu sisi tunaweza kuona sayari tano kwa wakati mmoja. Ukiangalia angani baada ya saa mbili usiku, Zuhura na Sambula zina tua katika upeo wa Magharibi. Wakati huo, sayari ya Mirihi (Mars) inang’aa kwa rangi nyekundu kali upande wa Mashariki. Wakati huo huo, sayari ya Zohali (Saturn) inaanza kuchomoza kwenye upeo wa Mashariki.