kupatwakwamwezi

Kupatwa Kwa Mwezi

Rudi - home

Kupatwa kwa mwezi wote alfajiri ya Alhamisi tarehe 21 February 2008 ni tukio la kipekee kwa namna mbalimbali. Ni tukio la mwisho la namna hiyo kwa zaidi ya miaka miwili, kwa sababu hakutatokea tena kupatwa kwa mwezi wote mpaka Desemba 2010. Zaidi ni kwamba ni matukio mawaili sawia ambapo utaweza hata kuelwa kwa nini mwezi au jua hupatwa.

Alfajiri ya siku ya kupatwa kwa mwezi wakati jua linapochomoza saa 12:30 asubuhi, utaweza kuona mwezi wote umepatwa upande wa magharibi. Toka nje usimame kwenye nagazi au uwanja wa wazi. Wakati huo, ukiangalia jua linalochomoza upande wako wa kulia, fikira tufe lenye ukubwa wa kilomita milioni moja na nusu likiwaka moto wa nuklia liktokeza upande wa mashariki. Tufe hili kubwa linloangaza liko umbali wa kilomita milioni 150 kutoka ulipo (duniani), upande wako wa kulia.

Sasa ukiangalia kushoto, utaona mwanga wa rangi chungwa wa mwezi uliopatwa, ukitua na kuzama kwenye upeo. Mwezi ni tufe la ukubwa wa kilomita 3,500 za mchanga na mawe na uko umbali wa kilomita 300,00 upande wako wa kushoto. Wewe ukiwa katikati hapa duniani, sasa unaweza kuona jua linalowaka likiweka kivuli kikubwa cha dunia kwenye mwezi mdogo na kuuziba kabisa na kusababisha kupatwa kama inavyoonekana katika mchoro wa hapa chini (kaw hisani ya Fred Espenak, 2000, http://www.mreclipse.com/Special/LEprimer.html,)

Kupatwa kwa mwezi hutokea wakati wa Mwezi Mpevu kwa sababu huo ni wakati ambapo jua, dunia na mwezi vinaweza kujipanga katika mstari ulionyooka na kivuli cha dunia kinaweza kuangukia juu ya mwezi.

Wakati wa alfajiri ya tarehe 21, mnamo saa 9:35 wakati bado usiku, mwezi kwanza utaingia katika kivuli chepesi ambacho hatuwezi kuona mabadiliko yoyote ya sura au mwonekano wa mwezi. Lakini ifikapo saa 10.43 asubuhi, mwezi utaingia katika kivuli cheusi cha giza na kuanza kuliwa na kuonyesha sura ya hilali (mwezi mchanga). Ifikapo saa 12 kamili asubuhi mwezi tayari utakukwa umemezwa na kivuli kitakachouziba mwezi wote.

Kutokana na ulingano wa mwanga unaoakisiwa kutoka katika mwezi, kivuli kinaonekana cheusi kabisa wakati unapofunikwa kiasi. Hata hivyo mara tu baada ya mwezi kufunikwa wote, kivuli ghafla kinaonyesha mng’aro ambao kwa kawaida inakuwa rangi nyekundu ya shaba. Rangi hii hutokana na mwanga uliopenyea kupitia anga la dunia na kuchepukia katika sehemu ya kivuli. Rangi ya dhahabu iliyokoza inaonyesha kuwa anga la dunia halina vichafuzi. Hata hivyo kama kuna vumbi lolote, moshi au chembechembe zozote zinazochafua anga la dunia, mwezi utakuwa na rangi ya kijivu. Kwetu sisi, kwa kuwa mara hii kupatwa kwa mwezi kunatokea karibu sana na maawio ya jua, tarajia rangi iwe nyepesi kwa sababu ya mwanga wa alafajiri. Hata hivyo kwa upande wa magharibi litakuwa giza kiasi cha kukuwezesha kufurahia kuona rangi ya kuvutia katika mwezi.

Watazamaji wa maeneo ya mwambao hawataweza kuona kukamilika tukio lote. Lakini walioko katika maeneo ya mpaka wa magharibi kama vile Kigoma wataweza kuona mwisho wa kupatwa-kabisa saa 12:52 asubuhi. Baada ya hapo mwezi utaingia katika kivuli chepesi na hilali angavu itaanza kujitokeza hadi mwezi wote utakuwa umeachiwa mnamo saa 2:10 asubuhi. Nchini Tanzania hatutapata bahati ya kuona sehemu ya mwisho ya tukio kwa sababu jua litakuwa limeeneza mwanga angani. Kupatwa kutamalizika kabisa saa 4:18 asubuhi wakati sote tukiwa katika shughuli za kazi.

Kupatwa kwa mwezi ni salama kabisa kuangalia kwa sababu mwanga unaotoka katika mwezi ni mwanga ulioakisiwa. Tumia muda kuangalia kupatwa huku hata kama kutamaanisha kupoteza kidogo usingizi wako. Itakusaidia kuelewa nini kinachotokea katika sehemu za Ulimwengu ambazo hatuwezi kufikia. Wakati mwingine wa kupata bahati hii ni baada ya miaka karibu mitatu.

Dkt Noorali Jiwaji

19 Februari 2008

Rudi - home