ALIYEKUWA kiongozi wa Mungiki, Maina Njenga, anajiandaa kuwa mhusika mkuu wa siasa za eneo la Mlima Kenya huku akitangaza nia yake ya kupatia jamii za eneo hilo mwelekeo katika siku zijazo.
Haya yanajiri baada ya uamuzi wa hivi majuzi wa mahakama uliomwondolea tuhuma za kuhusika na makundi ya wahalifu, shtaka ambalo amekuwa akikanusha mara kwa mara.
Bw Njenga anaamini kuwa wakati umefika kwa eneo la Mlima Kenya kuamua mkondo wake wa kisiasa na ameahidi kutoa tangazo kuu mnamo Januari 2025 kuhusu maono yake kwa maslahi ya jamii.
“Ninataka kuwaambia watu wetu kuwa watulivu kwani tunasuka mipango bora zaidi kwao. Tutatangaza mwelekeo ambao nchi inapaswa kuchukua Januari,” akasema Bw Njenga akiwasihi watu wa Mlima Kenya kutopoteza matumaini na kusisitiza kuwa eneo hilo lina viongozi wenye uwezo na ambao wako tayari kujitokeza kuliongoza.
Tangazo lijalo la Bw Njenga linafuatia tamko sawa na la Naibu Rais aliyetimuliwa Rigathi Gachagua na kuangazia ushindani wa kisiasa unaoendelea katika eneo hilo la Mlima Kenya.Tangu uchaguzi mkuu wa Agosti 2022 uliokuwa na ushindani mkali ufanyike, mvutano kati ya Bw Njenga na Bw Gachagua umedhihirika wazi.
Bw Gachagua alipochaguliwa kuwa Naibu wa Rais William Ruto, alimshutumu Bw Njenga kwa kuwahadaa vijana wa eneo hilo na kuwaingiza katika makundi ya wahalifu.Akimjibu, Bw Njenga alidai kuwa Bw Gachagua alikuwa akitumia rasilimali za serikali kuwalenga na kuwahangaisha vijana wa eneo hilo.
Kufuatia ushindi wake wa hivi majuzi katika mahakama ya Nakuru, Bw Njenga anashikilia kuwa mashtaka dhidi yake yalichochewa kisiasa. Katika shambulio lililomlenga Bw Gachagua, alidokeza kwamba wale waliotaka kumwangusha sasa wanakabiliwa na mashtaka.
“Nina furaha kuwa niko huru kwa sababu tuliundiwa njama na baadhi ya watu ingawa wao ndio sasa wanapambana na kesi kama walivyonifanyia,” alisema katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo
.Huku akilenga siasa za Mlima Kenya, Bw Njenga anatafuta uungwaji mkono na vijana ambao anasema kuwa watakuwa muhimu katika uchaguzi wa 2027. Ametoa wito kwa vijana kulinda vitambulisho vyao na kuwa tayari kupiga kura.
“Ninataka kutoa wito kwa vijana wote kwenda kuchukua vitambulisho vyao ili kufanya sauti zao kusikika na kuwa za kuhesabiwa ili wapate mabadiliko wanayohitaji. Tuko nyuma yao na tutawaunga mkono katika mchakato huu,” alisema.
Ingawa aliwania kiti cha Seneti ya Laikipia bila mafanikio kwa tikiti ya KANU katika uchaguzi uliopita wa 2022, hakubainisha ikiwa atawania kiti hicho.Hata hivyo, alisema angali katika muungano wa Azimio la Umoja ambao anaamini kuwa ndio chombo sahihi cha uongozi mbadala nchini Kenya.
‘Niko pamoja na viongozi wengine wa Azimio akiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na kinara wa ODM Raila Odinga, ambao tunaunga mkono kupata kiti cha mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika,’ akabainisha.
Kujitokeza kwa Njenga na Gachagua kuwania ubabe wa siasa za Mlima Kenya , ushindani mkali unatazamiwa katika eneo hilo na nchi kwa jumla.
KINARA wa ODM Raila Odinga ameunga Seneti kutaka serikali za kaunti zitengewe Sh400 bilioni huku akishutumu Bunge la Kitaifa kwa kuhujumu ugatuzi.
Bunge la Kitaifa na Seneti kwa sasa zinavutana vikali kuhusu mgao kwa serikali zote za kaunti 47. Maseneta wanataka kaunti zimegewe Sh400 bilioni huku Wabunge wakipendekeza Sh380 bilioni.
Mzozo kuhusu tofauti ya Sh20 bilioni umeendelea hata baada ya kuundwa kwa kamati ya upatanishi ya wanachama 18 ambayo inajumuisha wanachama sawa kutoka mabunge hayo mawili.
Bw Odinga alisema inashangaza kwamba, Bunge lilikuwa likishinikiza kupunguza kiwango cha pesa za mgao wa kaunti. Alilinganisha hatua ya wabunge hao na kunyonga kaunti na kuziua pole pole.
Alisema sheria inatengea kaunti angalau asilimia 15 ya Mapato ya Kitaifa na kusema Sh400 bilioni zilizopendekezwa na Seneti zinawakilisha asilimia 15 ya Mapato ya Kitaifa.
Alisema Bunge lilipendekeza marekebisho ya Sheria ya Ugavi wa Mapato, ambapo wanapendekeza Sh380 bilioni kwa kaunti, tofauti na Sh400 bilioni ambazo tayari zimeainishwa kwenye Sheria ambayo inatumika kwa sasa.
‘Msukosuko wa sasa na majaribio ya kupunguza mgao unaonyesha hatari ya kurudisha nyuma ugatuzi. Ninawaomba wabunge wetu wawe wawezeshaji wa ugatuzi na kukataa kushirikiana na wale wanaoazimia kuua ugatuzi,” akasema Bw Odinga.
Akihutubia wanahabari Ijumaa katika afisi yake ya Nairobi, Bw Odinga aliwataja Wabunge kama wachoyo kwa jaribio lao la kudhibiti mgao wa kaunti huku wakati huo huo wakimezea mate pesa zaidi kuwa chini ya usimamizi wao.
Waziri Mkuu huyo wa zamani alifichua kuwa, mbali na kudhibiti Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) na Hazina wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Usawa, wabunge walikuwa wakipanga njama ya kudhibiti Hazina ya Ushuru wa Kukarabati Barabara (RMLF).
Aliwashutumu wabunge hao kwa kutaka kuanzisha, kutekeleza miradi na kuisimamia kwa wakati mmoja.
Alisema “utekelezaji wa miradi haujawahi kuwa na kamwe hauwezi kuwa kazi ya wabunge bila kuleta mgongano mkubwa wa uwajibikaji katika mfumo wetu wa utawala kwa hasara yetu sote.”
Alisema ni aibu kuwa, baadhi ya wabunge hao wenyewe ni wanakandarasi katika miradi inayofadhiliwa na NG-CDF.’Ukweli usiofichika ni kwamba, mzozo huu ni kuhusu kunyakua mamlaka na kuhujumu katiba,’ alisema Bw Odinga.
“Bunge linatunga sheria, na kuhakikisha sheria zinatekelezwa na kufuatwa. Ni kutokana na hali hii ambapo mzozo unaoendelea kati ya mabunge yetu mawili kuhusu mgao wa mapato ukiwa tisho, haufai na hauhitajiki.
Katiba tuliyoizindua mwaka wa 2010 inaelekeza jinsi serikali na nchi yetu inavyofanya kazi,” alisema.
Alisema mzozo huo tayari unatishia kusimamisha shughuli na utoaji wa huduma katika kaunti. Alisema kaunti tayari zina matatizo na haziwezi tena kufadhili huduma muhimu.
“Bunge la Kitaifa linajitahidi kupunguza mgao wa mapato kwa kaunti, kwa kupuuza kabisa katiba na mapendekezo ya Seneti. Hatua hii sio tu kinyume cha sheria na kinyume cha katiba, bali inaweka historia hatari sana ambayo, ikiruhusiwa , itasababisha kukabwa koo polepole lakini kwa uthabiti na hatimaye kuua kaunti,” akasema.
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Ahmed Abdullahi Alhamisi alisema mzozo huo unaendelea kuumiza kaunti, huku shughuli zikikwama kwani pesa zinazotarajiwa kutoka kwa serikali ya kitaifa zimecheleweshwa
.’Ninataka Wakenya wajue kuwa kaunti ziko kwenye shida, haziwezi kufanya maamuzi, haziwezi kukamilisha michakato ya bajeti kwa sababu ya ukosefu wa Sheria ya Ugavi wa mapato kwa Kaunti,’ alisema Bw Abdullahi.
WABUNGE kutoka eneo la Kati mwa Kenya waliomsaidia Rais William Ruto kutimiza ajenda yake ya kumtimua aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua, sasa wanakabiliwa na wakati mgumu katika maeneo bunge yao.
Wakazi wa maeneo hayo wanawashambulia kwa maneno kwa kuunga mkono kutimuliwa kwa Bw Gachagua na nafasi yake kupewa Profesa Kithure Kindiki.
Kwa upande wake, Bw Gachagua amewataka wafuasi wake kuwaadhibu wabunge hao aliowataja kama wasaliti kwa kukaidi msimamo wa wapiga kura na kuunga mkono hoja ya kumwondoa afisini iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Bw Mwengi Mutuse.
Hali hii huenda ikaathiri nafasi ya wabunge hao kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Mnamo Jumatatu, Mbunge wa Nyeri Mjini, Bw Dancan Mathenge, alikabiliwa na wakazi wenye hasira waliomzomea vikali wakimtaja kama “msaliti”.
Alishindwa kabisa kuwahutubia wakazi hao hali iliyomlazimu kuondoka eneo hilo haraka baada ya idadi ya watu waliokuwa wakimzomea kuongezeka.
Hili sio tukio la kipekee kwa kuwa wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya waliomsaidia Rais Ruto kumtimua Bw Gachagua wanapitia wakati mgumu kwa kushambuliwa kwa maneno kila mara katika maeneo ya umma na kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii.
Juzi, wazee sita walikutana katika kaunti ndogo ya Kigumo na kuamua hadharani kumlaani Mbunge Mwakilishi wa Murang’a, Bi Betty Maina ambaye ni hasidi mkubwa wa Bw Gachagua.
Wakiongozwa na Mzee Mungai Njama, wazee hao walifanya matambiko ambapo walivunja vibuyu, nyungu na njele wakiapa kuwa mustakabali wa kisiasa wa Bi Maina utasambaratika.
Lakini Bi Maina alijibu kwa kusema hivi: “Wale waliowalipa pesa wazee ndipo wanilaani wataishia kujilaani wao wenyewe.”
Ili kuzuia kushambuliwa kila mara kupitia mitandao ya kujamii, Mwenyekiti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Bi Cecily Mbarire, ameamua kuzima sehemu ya maoni katika akaunti zake za mitandao ya kujamii.
Msururu huu wa mashambulio dhidi ya wanasiasa wa Mlima Kenya ambao walimsaliti Bw Gachagua hautakoma hivi karibuni, kulingana na Mbunge wa zamani wa Bahati, Bw Kimani Ngunjiri.
“Viongozi wanapaswa kuheshimu maoni na misimamo ya wapiga kura. Hitaji la ushirikishaji wa maoni kutoka kwa wananchi ni la kikatiba na linafaa kuheshimiwa,” anaongeza.
Bw Ngunjiri anakumbuka kisa cha Oktoba 11, 2024, siku tatu baada ya Bunge la Kitaifa kupitisha hoja ya kumtimua Bw Gachagua, wabunge wandani wa Rais Ruto walizomewa katika hafla ya mazishi katika eneo bunge la Bahati.
Mazishi hayo ya kakake mbunge wa eneo hilo, Bi Irene Njoki, Henry Gachie, yaligeuzwa kuwa jukwaa la kutoa kauli za kuipinga serikali ya Kenya Kwanza.
Ilimlazimu Gavana wa Nakuru, Bi Susan Kihika kunyenyekea na kuwaomba waombolezaji wamruhusu kusoma risala za rambirambi kutoka kwa Rais Ruto.
Lakini wabunge walioandamana naye walizimwa kabisa kuwatuhutubia waomboleza walioonekana kukerwa na hatua yao ya kuuunga mkono hoja ya kumtimua Gachagua.
Waliozimwa kuzungumza ni pamoja na Mbunge wa Ndia George Kariuki, Sabina Chege (Mbunge Maalum), Anne Wamuratha (Mbunge Mwakilishi wa Kiambu), Rahab Mukami (Mbunge Mwakilishi wa Nyeri).
Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi ambaye pia alikatazwa kuzungumza, baadaye aliwalaumu watu fulani, ambao hakuwataja majina, kwa kuwalipa waombolezaji wawazomee.